Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray amesema matumizi ya mifumo ya TEHAMA Serikalini yanaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza Mei 18, 2026 baada ya kutembelea Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (eGovRIDC) Jijini Dodoma, Mhe. Qwaray amesema mageuzi ya kidijiti si chaguo tena bali ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijiti ili kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza ukusanyaji wa mapato pamoja na kupunguza urasimu na vitendo vya rushwa.
Aidha, amesema matumizi ya mifumo hiyo yamesaidia kuongeza uwajibikaji katika utumishi wa umma pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe.Qwaray pia ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuendelea kubuni mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa e-Mrejesho unaowezesha wananchi kuwasilisha malalamiko, maoni na pongezi kwa taasisi za umma pamoja na Dirisha la Huduma za Serikali.
Sambamba na hayo, ameitaka e-GA kuendelea kushirikiana na vyuo vikuu, taasisi za tafiti pamoja na sekta binafsi ili kuongeza ubunifu wa teknolojia unaoweza kutatua changamoto za wananchi na taasisi za Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba amesema kituo cha eGovRIDC kilianzishwa kwa lengo la kukuza tafiti, ubunifu na kuwajengea uwezo vijana wabunifu katika sekta ya TEHAMA kwa ajili ya kuboresha huduma za Serikali Mtandao.



0 Comments