Makamu wa Rais awasili New York kumwakilisha Rais Samia UNGA81

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias Ndejembi, amewasili jijini New York nchini Marekani, ambako atamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA81.

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu maendeleo, uchumi, siasa, mazingira, haki za binadamu na changamoto nyingine za kimataifa.

Mhe. Ndejembi amewasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Togolani Mavura, pamoja na maafisa wengine.

Mkutano wa mwaka huu unaongozwa na kaulimbiu “Kurudisha Imani, Kusimamia Mabadiliko: Umoja wa Mataifa Unaohudumia Wote,” inayosisitiza umuhimu wa kujenga upya uaminifu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa.

Aidha, mjadala wa mkutano huo unatarajiwa kugusa mabadiliko yanayoendelea duniani, ikiwemo maendeleo ya teknolojia na matumizi ya akili unde (AI), pamoja na changamoto za maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.

Post a Comment

0 Comments