Watumiaji wa bahari, mito na maziwa wametakiwa kuzingatia utunzaji wa mazingira na usalama wa shughuli za usafirishaji majini, kwa kuwa uharibifu wa rasilimali hizo unaweza kuhatarisha maisha ya wananchi, miundombinu na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhandisi Ally Saidi Bakari, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi wa Zanzibar katika uzinduzi wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yaliyofanyika mkoani Tanga.
Mhandisi Ally amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za maji, ikiwemo bahari, mito na maziwa, ambazo ni chanzo cha ajira na kipato kwa wananchi kupitia uvuvi, utalii, biashara, usafirishaji, kilimo cha mwani na shughuli nyingine za uchumi wa bluu.
Amesema ni muhimu fursa zinazotokana na rasilimali hizo kutumika kukuza uchumi, huku hatua za kulinda mazingira na kuhakikisha usalama wa usafiri majini zikiimarishwa.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari na usafirishaji majini, akitaja maboresho yanayoendelea katika Bandari za Tanga na Zanzibar pamoja na miundombinu ya usafiri katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini kabla na wakati wa matumizi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza ajali na kulinda maisha ya abiria pamoja na mali zao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, Mtumwa Said Sandal, amesema uhifadhi wa mazingira ya bahari na kuhakikisha usalama wake ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali zinazopatikana baharini.
Sandal amesema matumizi endelevu ya rasilimali za bahari yanahitaji ushirikiano wa Serikali, wadau na wananchi katika kulinda mazingira na kuhakikisha shughuli zinazofanyika baharini haziathiri uendelevu wa rasilimali hizo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, amesema Tanga imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kutokana na fursa nyingi za kiuchumi zinazotokana na jiografia ya mkoa huo wenye mwambao wa bahari.
Mchatta amesema Tanga inaendelea kuwa kitovu cha shughuli za uchumi wa bluu, ikiwemo uvuvi, utalii, biashara na shughuli nyingine zinazohusiana na matumizi ya rasilimali za bahari.
Amesema maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Tanga yameongeza shughuli za kiuchumi, huku idadi ya meli zinazofika bandarini hapo ikiongezeka hadi takribani meli 17 kwa mwezi, kutoka meli moja kwa mwezi katika kipindi cha nyuma.



0 Comments