Serikali yawaonya Wafanyabiashara wadanganyifu kwenye zao la Mkonge

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameonya wafanyabiashara wa mkonge wanaodaiwa kufanya udanganyifu katika masoko ya nje, akisema Serikali haitavumilia vitendo vinavyoharibu uaminifu na taswira ya Tanzania katika biashara ya kimataifa.

Londo amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakichukua fedha kutoka kwa wanunuzi wa nje bila kupeleka mizigo waliyoahidi, hali ambayo imeanza kuathiri wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kwa kufuata sheria na taratibu.

Ametoa kauli hiyo jijini Tanga wakati wa kikao kazi kati ya Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Chama cha Wakulima wa Mkonge (SAT) na wafanyabiashara wa zao hilo.

Amesema Tanzania inaendesha uchumi wa soko huria, lakini uhuru huo haupaswi kutumiwa kama fursa ya kufanya biashara kinyume cha sheria au kukiuka misingi ya uaminifu katika masoko ya kimataifa.

“Nimesikia hapa wafanyabiashara wakilalamika kwamba wakati mwingine wanataka kukamatwa kwa sababu kuna baadhi ya wafanyabiashara wamefanya udanganyifu kwenye soko. Mtu akifanya hivyo anashindwa kujua kwamba huku nje yeye anatambulika kama Tanzania na wala si kampuni yake,” amesema.

Londo amesema vitendo hivyo vinaweza kulazimisha Serikali kutumia muda na rasilimali kurejesha uaminifu wa nchi katika masoko ya kimataifa, huku vikitoa taswira mbaya kwa wafanyabiashara wanaofuata taratibu.

Kutokana na hali hiyo, ameiagiza TSB, kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao hilo, kuchukua hatua za haraka dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kufanya udanganyifu.

“Pamoja na kwamba Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, hatuwezi kuvumilia hilo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TSB, Saddy Kambona, amesema changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kuchukua fedha kutoka kwa wanunuzi wa nje bila kupeleka bidhaa ni miongoni mwa malalamiko aliyokutana nayo katika ziara zake kwenye masoko ya mkonge duniani.

“Kwenye ziara yangu nimekutana na malalamiko kwamba kuna wafanyabiashara wamechukua fedha halafu wameshindwa kupeleka mizigo. Watu wanafanya udanganyifu kwenye masoko ya nje,” amesema Kambona.

Amesema wafanyabiashara watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao.

Kambona amesema hatua hizo zinalenga kulinda uaminifu wa biashara ya mkonge kutoka Tanzania na kuhakikisha vitendo vya watu wachache haviathiri wafanyabiashara wanaofuata sheria pamoja na soko la zao hilo katika masoko ya kimataifa.

Post a Comment

0 Comments