Na Mwandishi Wetu, Moscow
KAMPUNI ya Mkuyu Africa ni miongoni mwa wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania walioshiriki katika mazungumzo ya uwekezaji na biashara yaliyowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wa Urusi jijini Moscow.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Four Seasons, pembezoni mwa Mkutano wa Russia–Africa Summit, yalilenga kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za nishati, kilimo, madini, ujenzi na miundombinu.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, alisema ushiriki wao umetoa fursa ya kujenga mahusiano ya kibiashara, kubadilishana uzoefu na kukutana na wawekezaji wanaoweza kusaidia kukuza shughuli za kampuni hiyo.
“Tumefurahi kushiriki katika mkutano huu kwa sababu umetupa nafasi ya kukutana na wafanyabiashara mbalimbali, kujifunza kutoka kwao na kujenga mahusiano yatakayoweza kutusaidia kupanua wigo wa biashara zetu,” alisema Juneid.
Mkuyu Africa inajihusisha na uuzaji, upangishaji na ujenzi wa majengo ya makazi na biashara nchini Tanzania, ikiwa na miradi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, yakiwemo Kariakoo, Masaki, Msasani, Kawe, Mbezi na Mikocheni.
Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka Kenya, Peter Omong, alisema mikutano ya kimataifa ya uwekezaji ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara, hususan vijana, kupata washirika na kubaini fursa mpya za kukuza biashara zao.
Omong alisema kupitia mkutano huo amepata mahusiano mapya ya kibiashara, ikiwemo fursa katika biashara ya mafuta mazito na mbolea, hatua aliyoieleza kuwa muhimu katika kupanua mtandao wake wa biashara.
Aliongeza kuwa majukwaa hayo yanaweza kuchochea ukuaji wa biashara kwa kuwaunganisha wafanyabiashara na masoko, mitaji, teknolojia na washirika wapya.
Ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika katika majukwaa ya kimataifa unaendelea kutoa fursa za kujenga ushirikiano, kutafuta masoko mapya na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
.jpeg)
.jpeg)


0 Comments