
UNGUJA, ZANZIBAR: Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchangia kukuza nafasi ya Kiswahili katika sayansi, afya na teknolojia kupitia uwasilishaji wa utafiti unaochunguza makosa ya kifonolojia kwa watu wenye Afasia ya Broca na Wernicke, kwa kutumia uchimbaji data wa mitandao ya kijamii na mifumo ya Akili Mnemba (AI).
Utafiti huo wenye kichwa “Makosa ya Kifonolojia Kati ya Wagonjwa wa Afasia ya Broca na Wernicke Katika Lugha ya Kiswahili: Uchambuzi wa Kiisimu Tiba kwa Kutumia Uchimbaji Data wa Mitandao ya Kijamii na Mifumo ya Akili Mnemba” uliwasilishwa na Bi. Edelfrida Tibaija, Afisa Programu wa Sekta ya Utamaduni, Tume ya Taifa ya UNESCO, katika Kongamano la 10 la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika tarehe 11–12 Novemba 2026, Unguja, Zanzibar.

Makala hiyo iliandaliwa na Bi. Edelfrida kwa kushirikiana na Dkt. Ahmad Yahya Sovu wa Idara ya Lugha na Fasihi, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Kampasi ya Kivukoni, Dar es Salaam.
Utafiti huo umechunguza namna Afasia ya Broca na Wernicke zinavyoathiri matamshi ya wazungumzaji wa Kiswahili. Kwa kutumia sampuli ya machapisho 20 kutoka Instagram, pamoja na programu ya Praat, mifumo ya Utambuzi Kiotomatiki wa Usemi (ASR) na Akili Mnemba, utafiti ulibaini kuwa Afasia ya Broca hujitokeza zaidi kwa udondoshaji wa sauti, hasa katika viambishi awali vya nafsi na wakati, huku Afasia ya Wernicke ikihusishwa na ubadilishaji wa sauti na mabadiliko ya mpangilio wa silabi.

Matokeo hayo yanaonesha fursa ya kutumia teknolojia za kisasa katika kupanua tafiti za Isimu Tiba kwa lugha ya Kiswahili. Utafiti unapendekeza kuimarishwa kwa tafiti katika eneo hilo, ushirikiano kati ya wanaisimu na wataalamu wa afya, pamoja na kuendelezwa kwa teknolojia saidizi zinazoweza kusaidia uchambuzi wa changamoto za lugha na mawasiliano.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) lilikuwa jukwaa la kukutanisha wadau, watafiti na wataalamu wa Kiswahili kutoka maeneo mbalimbali ili kujadili maendeleo na matumizi ya lugha hiyo.

Ushiriki wa NATCOM kupitia uwasilishaji huo unaonesha dhamira ya Tume ya kuendeleza Kiswahili kama lugha ya maarifa, utafiti, sayansi na ubunifu, pamoja na kukuza matumizi yake katika ulimwengu wa kidijitali.
0 Comments