VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA TANGA WATOA WITO WA KULINDA AMANI

 

Viongozi wa vyama vya siasa katika Wilaya ya Tanga wamekutana na waandishi wa habari kwa lengo la kuhamasisha jamii kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo, wakisisitiza kuwa msingi wa maendeleo endelevu ni amani iliyodumu katika mkoa huo.

Mkutano huo umefanyika kama sehemu ya mikakati ya kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kijamii, huku viongozi wakibainisha umuhimu wa ushirikiano katika kutoa elimu juu ya madhara ya machafuko na faida za kudumisha utulivu.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Kamati ya Amani na Uratibu wa Vyombo vya Siasa Mkoa na Wilaya ya Tanga, Hemed Bakari, amesema kamati imejipanga kuhakikisha hakuna shughuli au matukio ya kisiasa yatakayochochea uvunjifu wa amani.

Bakari amesema kumekuwa na viashiria kadhaa vinavyoashiria uwezekano wa kuhamasisha maandamano katika baadhi ya maeneo, hali iliyowafanya waanze kutoa elimu ya mapema na kuzungumza na wadau ili kudhibiti mambo yasiende mahali pabaya.

Ameeleza kuwa maandamano yasiyo rasmi yanaweza kurejesha nyuma shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuleta hofu, uharibifu wa mali na kusababisha vurugu zisizo na tija kwa wananchi.

Katika ufafanuzi wake, Bakari amesema kamati hiyo inaendelea kushirikiana na viongozi wa mitaa, kata na jamii ili kuhakikisha ujumbe wa amani unawafikia wananchi wote bila kuacha pengo lolote.

Aidha, amewahakikishia wananchi wa Tanga kuwa ulinzi na utulivu wa mkoa uko imara, na kuwataka waendelee na shughuli zao bila wasiwasi huku wakiepuka kutishwa na taarifa zinazoenezwa bila uthibitisho.

Bakari pia amewataka vijana kutotumiwa vibaya katika masuala ya kisiasa, akisema mihemko isiyodhibitiwa imekuwa chanzo cha vijana wengi kupoteza mwelekeo na kushindwa kufikia malengo yao muhimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK) Mkoa wa Tanga, John Mtunguja, amepongeza jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuendelea kuwa karibu na viongozi wa vyama vya siasa kupitia majadiliano na mikutano ya pamoja.

Mtunguja amesema ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro na kuimarisha maelewano miongoni mwa vyama, akisisitiza kuwa mazungumzo na ushirikiano ndiyo njia sahihi ya kujenga taifa lenye umoja na utulivu wa kudumu.

Post a Comment

0 Comments