Mwanafunzi ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mwenzake Kisarika

 

Mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Kisarika, Nelson Charles Mkenda, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali mwanafunzi mwenzake, Vicent Thomas Mmary, ambaye baadaye alifariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea Agosti 28, 2026, majira ya saa 9:15 alasiri katika Shule ya Sekondari Kisarika, iliyopo Kitongoji cha Manushi, Kijiji cha Ongomauru, Kata ya Uru Kaskazini, Wilaya ya Moshi.

Kamanda Maigwa amesema awali kulitokea ugomvi kati ya wanafunzi hao, baada ya marehemu kumtuhumu mtuhumiwa kuhusika na wizi wa vitu mbalimbali katika mabweni ya shule hiyo.

Amesema Vicent alijeruhiwa kifuani kwa kitu chenye ncha kali na alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi kwa ajili ya matibabu.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kukamilisha taratibu za kisheria na kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewataka wananchi na wazazi kuwa watulivu wakati taratibu za kisheria zikiendelea dhidi ya watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote katika tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments