Mradi wa Tanzania FAST Health umezinduliwa katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, ambapo kata 10 zitanufaika na mradi huo unaolenga kuimarisha huduma za afya hususan kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 0 hadi 19 wanaoishi na VVU.
Akizindua mradi huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Japhet Simeyo amesema Serikali imejipanga kushirikiana na wadau katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama za afya.
Simeyo amesema lengo kuu la mradi huo ni kuongeza matumizi ya mbinu zinazotokana na ushahidi na zinazoweza kuendelezwa kwa muda mrefu katika kuibua kwa haraka watu wapya walioambukizwa VVU,hususan kupitia familia na jamii, pamoja na mfumo wa kugawana majukumu kwa watendaji wa afya.
Dkt.Mariana Mubelwa akizungumza katika uzinduzi wa mradi huoAmesema hatua hiyo inalenga kuziba mapengo yaliyopo katika utoaji wa huduma za VVU kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 0 hadi 19,huku mradi ukilenga pia kuhakikisha mwendelezo wa matibabu kwa kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa wanaopata huduma na kupunguza hali ya kukatisha au kuacha matibabu.
Aidha, amesema mradi utaimarisha mifumo ya afya kupitia uboreshaji wa takwimu, kuongeza uwezo wa watumishi wa afya, kuunganisha huduma, kushirikisha jamii pamoja na kuimarisha mifumo ya upatikanaji na usambazaji wa vifaa na dawa.
Miongoni mwa afua zitakazotekelezwa kupitia mradi huo ni upimaji wa VVU katika jamii na kwa watu waliokaribu na mtu aliyebainika kuwa na VVU, ufuatiliaji na uunganishaji wa wanaohitaji huduma na matibabu, mpango wa Mama Walezi (Mentor Mothers), kuanzisha na kuimarisha klabu za vijana balehe, elimu rika, vikundi vya msaada wa kisaikolojia pamoja na kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii.
Msimamizi wa Mradi wa Tanzania FAST Health Japhet Daudi akieleza namna mradi huo utakavyofanya kazi katika jamii.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA), likiwemo Mtandao wa Vijana Wanaoishi na VVU (NYP+), na unahudumia vituo 19 vya afya vilivyopo katika kata 10 za Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Tanzania FAST Health ni mradi wa miaka mitatu unaotekelezwa na Tanzania Health Promotion Support (THPS) kuanzia Juni 2026 hadi Juni 2029, kwa ufadhili wa ViiV Healthcare Positive Action, ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za VVU kwa watoto na vijana pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.



.jpeg)
.jpeg)
0 Comments