Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) wameanza hatua za kujenga ushirikiano wa kimkakati wenye lengo la kuongeza elimu kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji.
Hatua hiyo imekuja baada ya timu ya maofisa wa PSSSF kufanya ziara rasmi katika makao makuu ya muda ya TBN yaliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, na kufanya mazungumzo na viongozi wa mtandao huo.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili, hususan katika masuala ya habari, uelimishaji wa umma na usambazaji wa taarifa sahihi kuhusu mifumo ya pensheni pamoja na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo upo tayari kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu na kusambaza maarifa sahihi kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.
Hata hivyo, Msimbe alisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupatiwa kwanza mafunzo ya kina kuhusu shughuli, huduma na uendeshaji wa PSSSF ili waweze kufikisha taarifa sahihi kwa jamii.
Alieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi zaidi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara kutoka PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo imelenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari pamoja na kuangalia namna bora ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.
Aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi na hoja zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu pensheni na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo unajivunia historia, weledi na ufanisi katika sekta ya habari za kidijitali.
Alisema TBN ipo kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kusomeka vyema katika medani za kidijitali, sambamba na kuchochea na kupanua gurudumu la maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo uko tayari kutumia waandishi wake mahiri pamoja na majukwaa mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na za kuaminika.
Alisema taarifa hizo zitasaidia wananchi na wadau mbalimbali kupata uelewa unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF ulioongozwa na Abdul Njaidi ulijumuisha pia Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.
Kwa upande wa TBN, viongozi waliohudhuria walikuwa Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna, pamoja na Mdhamini wa mtandao huo, Issa Michuzi.


0 Comments