WAKULIMA BABATI WANUFAIKA NA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP)




Na; Mwandishi wetu – Babati

Wakulima wa vijiji vya Endakiso na Orng'adida vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara wameeleza kunufaika na Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kushirikina na Serikali na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, na wenye Ulemavu.

Kwa nyakati Tofauti wakulima kutoka vijiji hivyo wameyasema hayo tarehe 4 Septemba wakati wa ziara ya timu kutoka IFAD inayotathimini maendeleo ya utekelezaji Programu ya muda wa kati (MTR).

Wakulima hao waliweka bayana kuwa, Programu hiyo imeweza kuwaletea teknolojia ya kisasa ya Kilimo Mseto kwa kutumia Mbegu himilivu zinazoweza kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.


Akizungumza wakati wa Ziara hiyo Bw. Ramadhani Iddi Mfumbilo mkulima kutoka katika kijiji cha Mkombozi Kata ya Endasiko alisema, kupitia Programu hii wakulima wameweza kupata mbegu za mahindi aina ya situka na mbegu za lishe ambazo zimepandwa mashambani pamoja na mazao mengine kama vile labulabu ambayo yanaweza kurutubisha ardhi na kuzuia Mmomonyoko wa udongo.


“Majani hayo pia siyo rafiki kwa mifugo kama vile ng’ombe hivyo mifugo itakapovamia shamba la Mkulima si rahisi kuweza kula au kuharibu mazao, na yanakimbiza wadudu waharibifu wa mazao.” Aliendekea kufafanua.


Alibainisha kuwa, Mbegu hizi za Lishe zina uwezo mkubwa wa Kurutubisha Afya ya Familia hasa kwa watoto, kinamama wajazito, wazazi na wazee na pia zimesaidia kupunguza magonjwa ya Utapiamlo kwa watoto.

Aidha, Akiongelea mbegu za Jamii ya Mikunde yaani Maharage aina ya Jesca, alisema, Mbegu hizo zina virutubisho muhimu na vya kipekee hasa kwa watoto.


Kwa upande wake Bi Naseriani Joseph kutoka katika Kijiji cha Orng'adida Kata ya Qash mkulima wa mazao ya Lishe yanayolimwa katika bustani nyumbani maarufu kama '_Kitchen gardens_', alisema kuwa, kupitia Programu ya AFDP wakulima hao waliweza kupata Elimu na Mbegu bora za mazao ya lishe ambayo wanalima Nyumbani na wamepata manufaa mengi kama vile kuwepo kwa mboga nyumbani pamoja na kuwasaidia watoto shule na familia kwa ujumla pamoja na kuimarisha Afya ya familia na kuongeza kipato


“Wanawake tunapata mahitaji yetu muhimu kupitia kilimo hiki kwa upande wa mboga mboga na mazao ya mikunde, tumepata elimu ya maharage lishe tumepata mbegu na tumeyatumia, Maharage yale yameboreshwa yana viini lishe na madini chuma, hivyo afya za familia zinaimarika, natoa tuu wito kwa serikali kuongeza mbegu hizi maana ni adimu na zinazalishwa kwa uchache katika kata yetu. Alisema”


Wataalam hao wanaendelea na ziara hiyo kwa kutembela maeneo tofauti yanayotekeleza programu nchini katika sekta za Kilimo na Uvuvi.

Post a Comment

0 Comments