Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Emidius Kasunzu, amesema maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini yanahitaji wataalamu, wabunifu, wajasiriamali na watafiti wenye uwezo wa kutambua changamoto na kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo.
Amesema Tanzania inapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta hiyo, ikiwemo matumizi ya nishati safi, teknolojia za kidijitali na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa bandari.
Kasunzu ameyasema hayo jijini Tanga wakati akifungua warsha ya Siku ya Bahari Duniani 2026, iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa na kitaifa vinavyosimamia sekta ya usafiri wa majini.
Amesema miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika warsha hiyo ni kuimarisha usalama na ufanisi wa shughuli za usafiri wa majini, matumizi ya nishati safi na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa katika meli na bandari.
Ameongeza kuwa warsha hiyo inalenga pia kuimarisha ustawi, usalama na hifadhi ya kijamii kwa mabaharia, kuwaandaa wataalamu kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayokua kwa kasi, pamoja na kuboresha mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu.
Kwa mujibu wa Kasunzu, lengo ni kujenga sekta ya usafiri wa majini yenye ufanisi, usalama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi Zanzibar, Stella Katondo, amesema maadhimisho hayo pamoja na warsha yameandaliwa kwa lengo la kuhakikisha masuala ya ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira katika sekta ya usafiri wa majini yanapewa kipaumbele.
Katondo amesema ni muhimu kuhakikisha bahari, mito na vyanzo vingine vya maji vinatumika kwa namna inayozingatia mahitaji ya kizazi cha sasa, huku vikihifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Amesema Shirika la Kimataifa la Usafiri Majini (IMO) huweka miongozo mbalimbali ya usalama, ulinzi na uhifadhi wa mazingira ambayo Tanzania, kama mwanachama, inapaswa kuifuata na kuitekeleza.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (TASAC), Judith Kakongwe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, amesema warsha hiyo inatoa nafasi kwa Tanzania kutafakari utekelezaji wa mikataba ya kimataifa katika maeneo ya usalama, mazingira na mabaharia.
Kakongwe amesema Tanzania imeridhia mikataba 25 kati ya mikataba 50 ya kimataifa inayosimamia sekta hiyo, na kwamba inaendelea kupitia mikataba mingine ili kuhakikisha nchi haiwi nyuma katika utekelezaji wa viwango vinavyotumika kimataifa.
Amesema mikataba ambayo Tanzania imeridhia imewezesha kutengenezwa kwa sheria na kanuni mbalimbali zinazosaidia kusimamia sekta hiyo.
“Tunatoa elimu, tunatafakari na kufanya tathmini ya sheria tulizonazo, ikiwemo katika usajili wa meli, mabaharia, elimu zao na utekelezaji wa majukumu katika maeneo ya mazingira,” amesema.




0 Comments