Serikali imeendelea kuimarisha usalama katika usafiri wa majini kwa kuwekeza katika vyombo vya utafutaji na uokoaji, ikiwemo boti nne zinazotumika kukabiliana na majanga baharini.
Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanya zoezi la utafutaji na uokoaji katika Bahari ya Hindi, eneo la Raskazone jijini Tanga, kwa lengo la kupima utayari wa vyombo na wataalamu.
Zoezi hilo limehusisha majaribio ya uwezo wa kukabiliana na matukio mbalimbali yanayoweza kutokea baharini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuokoa maisha na mali.
Hatua hiyo inalenga pia kuhakikisha wataalamu na vyombo vya utafutaji na uokoaji vinakuwa tayari kutoa huduma kwa wakati pale yanapotokea majanga katika maeneo ya majini.
Akizungumza baada ya kukagua zoezi hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama na huduma katika sekta ya usafiri wa majini.
Amesema uwekezaji huo unaongeza uwezo wa kutoa msaada kwa waathirika na kuimarisha utayari wa kukabiliana na majanga baharini.
Boti hizo zimegawanywa katika maeneo mbalimbali ambapo moja ipo mkoani Tanga,nyingine Kigoma na mbili zikiwa katika Ziwa Victoria.
Miongoni mwa vyombo hivyo pia kuna boti maalumu inayoweza kutumika kutoa huduma za afya kwa waathirika wakati wa dharura zinazotokea majini.







0 Comments