Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mheshimiwa Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Nne kuandika barua kwa Katibu Mkuu TAMISEMI mhandisi Joseph Nyamhanga kujieleza ni kwanini walishindwa kuwaruhusu wakuu wa shule kuhudhuria mkutano wao wa mwaka.
Waziri Jafo, ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania bara (TAHOSSA) unaofanyika jijini Dodoma.
Amebainisha, kuwa mkutano kama huo ndiyo sehemu ambayo serikali inatumia kutoa maagizo kwa wakuu wa shule katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya elimu katika maeneo yao.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imetoa fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya elimu ambayo wasimamizi wakuu ni wakuu wa shule za sekondari hivyo ushiriki wao katika mkutano huo ni jambo la lazima.
“Kuna kiasi kikubwa cha fedha serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya shule nchini na wasimamizi ni nyinyi wakuu wa shule hivyo uwepo wenu hapa na sisi serikali tunapata fursa yakutoa maagizo yetu lakini sasa kuna baadhi ya wakurugenzi wameshindwa kutoa vibali kwa wakuu wa shule” amesema Jafo.
Wakurugenzi ambao hawakutoa ruhusa kwa wakuu wa shule za sekondari kwamujibu wa Jafo ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Kahama DC, Kologwe DC pamoja na Sikonge.
Kutoka na hali hiyo Waziri Jafo, amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga kuwachukulia hatua wakurugenzi hao haraka.
“Namwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Nyamhanga kuhakikisha wakurugenzi hawa wanatoa maelezo kwanini wameshindwa kutoa ruhusa, na hatua hizo zichukuliwe haraka”amesema.
Vile vile Jafo, amewaagiza wakurugenzi Halmashauri zote hapa nchini, kuhakikisha kuwa mwaka 2021 wanasimamia upimaji wa maeneo ya shule ili kupata hati miliki na kuondoa migogoro ya ardhi.
Amebainisha katika mwaka wa Fedha 2020/21 serikali imetenga zaidi ya Sh. bilioni 68 kwajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,088 na kiasi cha Sh. bilioni 42.3 kwajili ya ujenzi wa vyumba vya maabara ili kuwezesha vijana wetu wanaosoma masomo ya sayansi kujifunza kwa vitendo”
0 Comments