MSIKIMBILIE KWA WAGANGA WA KIENYEJI


Na Dege Masoli, KILINDI.


Mkuu wa Wilaya  ya Kilindi Mkoa wa Tanga, Abel Basalama
amewatahadharisha wananchi wa Wilaya hiyo kuhusu tabia ya kukimbilia
kwa waganga wa tiba asili wanapougua na kuwaonya waganga hao kuacha
kuwang’ang’ania wagonjwa hao na badala yake wawashauri  kuwahi
hospitalini ili kuepusha vifo visivyokuwa na lazima.

Busalama alitoa ovyo hilo jana wakati akizindua kampeni ya wiki ya
mwanzo ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa ICHF uliyoboreshwa
uliyofanyika katika kijiji cha Kwamba Kata ya Songe Wilaya ya Kilindi.

Pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa tatizo la
watu kuchelewa kufika katika huduma za afya kwa wakati limekuwa chanzo
 cha vifo visivyo na lazima.

Aliwatahadharisha wananchi hao kuwa wanapougua kwanza wafike kwenye
zahanati na inaposhindikana wanaweza kuangalia njia nyingine ikiwemo
kwenda katika  tiba mbadala.

“Mimi sipingani na tiba mbadala, lakini ninachoshauri huduma hiyo iwe
baada ya huduma ya hospitali, madaktari wetu watakapobaini tatizo
linalokusumbua siyo la hospitali watakueleza na wewe sasa angalia
kwingineko” alisema Basalama.
Alieleza athari za watu kukimbilia kwenye tiba asili badala ya
hospitali kuwa ni vifo  ambavyo  visingetokea kwani  mara nyingi
wagonjwa hao hufikishwa hospitali wakiwa wameshachoka na wamechelewa.

Kwa upande wa ICHF, Busalama aliwataka wananchi kujiunga nao ili
kujiondolea  mawazo  pale wanapoumwa ama kuuguliwa  kipindi ambacho
hawana pesa na kwamba suluhu yake ni kuwa na kadi  hiyo ya matibabu
bure.

Katika taarifa iliyosomwa na mratibu wa ICHF Wilaya ya Kilindi, Modi
Mngumi  ilieleza mafanikio ya mfuko huo tangu kuanza utekelezwaji wake
mwaka 2019 ni pamoja na kufikisha elimu kwa wananchi wa Kata 21 za
Wilaya hiyo.

Mngumi alisema kutokana na elimu hiyo wananchi wametambua umuhimu wa
mfuko  na wigo wa mipaka ya huduma kuongezeka kutoka katika kituo kaya
ilipojiandikisha hadi ngazi ya Mkoa na nje yake na hivyo jumla ya watu
18,136 wamefikiwa  na elimu hiyo.

“Kupitia uhamasishaji huo, kaya zaidi ya 2000  zimejiunga na mfuko
huo, lengo la kiwilaya likiwa ni  kuandikisha kaya 16,714 kwa mwaka”
alieleza Mngumi.
Naye mratibu wa ICHF Mkoa wa Tanga, Imani  Clemence alieleza lengo la
Mkoa kuwa ni kusajiri kaya 146,954 sawa na asilimia 30 hadi ifikapo
juni 30 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments