Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahaman Shiloow akizungumza na Wafanyabiashara
Mwenyekiti wa Soko la Mlango wa Chuma
Diwani Kata ya Majengo Salim Perembo
Na Mashaka Mhando, Tanga
HALMASHAURI ya Jiji la Tanga, imepanga kutenga bajeti ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kujenga soko jipya la kisasa katika kata ya Majengo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kujionea uchakavu na ubovu wa miundombinu ya soko la Mlango wa Chuma, Meya wa Jiji hilo Abdulrahman Shillow alisema kuwa halmashauri katika bajeti yake ya mwaka 2022/2023 itatenga fedha hizo kwa awamu mbili.
Alisema kutokana na uchakavu aliojionea halmashuri kupeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 10 au 15 haziwezi kusaidia matatizo yaliyopo katika soko hilo, hivyo wataleta fedha za kutosha ili lijengwe upya.
Alisema unaweza kupeleka fedha hizo kwa nia njema lakini zikaliwa bure na wajanja ama zisitoshe kulifanyia ukarabati soko hilo ambalo kwa mazingira lilivyo sasa na kuwa kwake mjini, halileti sura nzuri kwa Jiji.
"Ndugu zangu nimeona hali ilivyo ni mbaya niwahakikishie kwamba tutajipanga katika bajeti ya mwaka 2022/23 kulitengea milioni 500 na baadae fedha kama hizo ili lijengwe na liwe na hadhi ya Jiji letu, " alisema Meya huyo.
Diwani wa Kata ya Majengo Salimu Perembo aliyeongoza na viongozi mbalimbali wa mitaa ya kata hiyo, alisema kwamba soko hilo hali yake siyo nzuri na kipindi cha mvua wafanyabiashara wanafanya biashara zao katika mazingira magumu.
Perembo alisema kuwa miundombinu ya soko hiyo hairidhishi kuhudumia wananchi ikiwemo choo kilichopo sokoni hapo hakina hadhi ya kuwahudumia wafanyabiashara hao pamoja na wateja wao.
"Mstahiki Meya soko letu siyo zuri miundombinu na mazingira yake ni mabaya, choo pia siyo kizuri, vichafu havina hadhi ya kuhudumia watu," alisema Perembo.
Awali mwenyekiti wa wafanyabiashara sokoni hapo, Hamza Mkemea alisema soko lao ambalo awali ilikuwa ni kilabu cha pombe za kienyeji, halijafanyia ukarabati wowote tangu litumike kuuza bidhaa mbalimbali.
Hata hivyo, alimpongeza diwani wao kwa kulitembelea mara kwa mara na kuona changamoto zao sokoni hapo na kwamba hatua ya kutembelea na Meya wameifurahia.
"Mheshimiwa Diwani tunakupongeza kwa hatua hizi, tumeanza kuona umuhimu wa kukuchagua kuwa diwani Wetu tunakuahidi hatutakuangusha tutakuwa na wewe bega kwa bega sababu unajali matatizo yetu, " alisema Mkemea.
0 Comments