JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA TANGA YAOMBA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU


Na.Mwandishi Wetu, Tanga

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Tanga imefanya dua maalum ya kuombea amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.

Dua hiyo imefanyika katika viwanja vya Lamore mjini Tanga na kuhudhuriwa na viongozi wa dini pamoja na wananchi wa kada mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kiroho,Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alisema lengo la dua hiyo ni kumkabidhi Mwenyezi Mungu mchakato mzima wa uchaguzi ili uwe wa amani, haki na utulivu. Alisisitiza kuwa Tanzania imejengwa katika misingi ya amani na upendo, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha thamani hiyo inaendelezwa.

“Tunamuomba Mungu alinde nchi yetu kipindi hiki cha uchaguzi. Tusiingie kwenye maneno ya uchochezi au migogoro, bali tuonyeshe ustaarabu na hekima kwa kupiga kura kwa utulivu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wao,viongozi wa dini walioshiriki katika dua hiyo waliwahimiza Watanzania kutambua kuwa chaguzi huja na kuisha, lakini amani ni urithi wa kudumu unaopaswa kulindwa na kila mmoja. Walisema migawanyiko ya kisiasa isiwagawe wananchi kwani wote ni ndugu wanaoshirikiana katika kujenga taifa moja.

Wazazi walioshiriki waliwataka vijana kuepuka kushawishiwa kufanya vurugu au kusambaza taarifa za uongo mitandaoni. Walisisitiza kwamba jukumu la vijana ni kuwa mabalozi wa amani na kuchagua viongozi wanaolenga maendeleo ya nchi.

Katika dua hiyo, walimwomba Mwenyezi Mungu awape hekima na busara viongozi wote wa kisiasa, wagombea, na wasimamizi wa uchaguzi, ili kuhakikisha mchakato mzima unafanyika kwa uwazi na haki.

Aidha, walimuomba Mungu kumzuia yeyote atakayepanga kuleta vurugu au kuchafua hali ya amani nchini asifanikiwe katika mipango yake, ili Watanzania wote wapige kura wakiwa salama na wenye matumaini.

Jumuiya hiyo pia imeahidi kuendelea na mikutano ya kiroho na hamasa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tanga, ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuhimiza wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu.

Mwishoni mwa tukio hilo, dua maalum ilisomwa kwa ajili ya kulibariki Taifa, viongozi wake, na wananchi wote, ikihitimishwa kwa wito wa kudumisha umoja, mshikamano, na uzalendo katika kipindi chote cha uchaguzi.

Post a Comment

0 Comments