Wenyejiwa eneo la Makorora, jijini Tanga, wameombwa kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Makorora, mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Said Mohamed aliwahimiza wananchi kuendelea kuiamini serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi chake cha uongozi.
Amesema uongozi wa Dkt. Samia umeleta mageuzi makubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uwezeshaji wa vijana, jambo linalopaswa kuungwa mkono kupitia kura.
Said pia amewataka wananchi wa Tanga kumpigia kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Kassim Amari, akieleza kuwa ni kiongozi mwenye maono ya maendeleo na anayejali wananchi.
Aidha, aliwahimiza wakazi wa Makorora kumchagua diwani wa kata hiyo kupitia CCM, akisema ushirikiano wa viongozi wote wa chama hicho utarahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
“Niseme tu, watu wote hapa Makorora tunajuana — tuichague CCM kwa maendeleo. Chama hiki kimefanya mengi, na bado kina mipango mizuri ya kuinua maisha yetu,” alisema Said wakati wa mkutano huo.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo waliipongeza serikali kwa jitihada zake katika kuboresha huduma za jamii, hasa ujenzi wa barabara na maboresho ya sekta ya elimu katika Jiji la Tanga.
Baadhi ya wananchi walisema wanaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi chini ya uongozi wa Rais Samia, na kuahidi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Walisema kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa CCM imeleta matumaini makubwa kwa wakazi wa Makorora na maeneo mengine ya Jiji la Tanga.
Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho, wakiwemo vijana na wazee wa Makorora, ambao waliapa kuendelea kuiunga mkono CCM kwa maendeleo endelevu ya taifa.
0 Comments