MWANA FA AZUNGUMZA NA WANANCHI WA KATA YA MASUGURU

Na Mwandishi Wetu, kata ya Masuguru

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amemuombea kura mgombea Urais Dkt Samia Suluhu Hassan mtaa wa Masuguru ambako aliishi akiwa mdogo baada ya kuzaliwa.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika mtaa wa Masuguru, kata ya Masuguru mbele kidogo ya nyumba aliyokuwa akiishi na bibi ake bint Ashraff ambaye Sasa ni marehemu.

MwanaFA alimkaribisha Katibu wa CCM wilaya ya Muheza Simon Leng'ese akimwambia mkutano huo unafanyika katika mtaa alioishi na kukulia wakati akiwa mdogo.

"Naomba nikukaribishe nyumbani Katibu Leng'ese hapa ni kwetu, hii nyumba ni ya Mzee Kishe, hii ya Kombo Maridadi, Ile ya Mzee Ngudu, halafu ya bi Joy,  Kombo Daffa, inafuatia ya Dkt Michael ya mama Yambi halafu kwa bint Ashraff ambapo ndipo nimekulia Mimi," alisema.

Alisema hapo ni nyumbani hata alipofika na wenzake watano kwenye kura za maoni kati ya kura 121 zilizopigwa alipata kura 101 hivyo ni uwanja wake wa kujidai.

Hata hivyo, aliwaomba wananchi wenzake wa mtaa huo waende wakapige kura Oktoba 29 kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan, yeye kijana wao waliemlea na diwani Mohamed Baghozah kwakuwa CCM katika kipindi kilichopita ilitekeleza vizuri ilani yake.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano Masuguru CCM ilifanya kazi kupitia mbunge huyo na Muheza kwa ujumla lakini pia heshima aliyopewa na Rais ya kumsaidia kazi za serikali nchini, nimewaheshimisha watu wa Masuguru na Muheza kwa ujumla.

"Nimekuja nyumbani kuwaomba tusifanye mzaha kura 4,805 za waliojiandikisha hapa Masuguru ambayo ni Moja ya kata iliyokuwa na watu wengi waliojiandikisha, mtoke mkachague wagombea wa CCM," alisema na kuwaomba, "Naomba mniheshimishe ndugu zangu mtoto mliyemlea amepevuka na anafanya kazi sawa sawa hawaangushi,".

MwanaFA alisema katika wakati wowote hakuna fedha nyingi zimekuja katika kata hiyo kama kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo jumla ya shilingi milioni 389.2 zilikuja kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alitaja fedha zilizokuja katika elimu ya msingi kuwa ni shilingi milioni 332.8 ambazo zilijenga madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo. Fedha hizo zilitekeleza miradi hiyo katika shule ya msingi Masuguru na Mkabala.

Kwa upande wa maji zililetwa kiasi cha shilingi milioni 31 ambazo zilikarabati miundombinu ya maji lakini pia shilingi milioni 20 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima katika eneo la shule ambapo kinasaidia wananchi wa maeneo jirani.

Kwa upande wa barabara alisema kuwa wamezichonga ikiwemo kujenga lami katika barabara inayoelekea Kwamkabala lengo barabara hiyo ifike Kerenge kata ya Tingeni.

Alisema kwamba katika mfuko wa Jimbo alitoa shilingi laki Tano shule ya msingi Masuguru.

Post a Comment

0 Comments