WANANCHI WA MTINDIRO WAFURIKA KWA MWANA FA AKIOMBA KURA ZA CCM

Mgombea Ubunge Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA akizungumza  katika Kijiji cha Mtindiro


Mgombea Ubunge Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA akizungumza na Wananchi katika Kijiji cha Mtindiro


**********************

Na.Mwandishi Wetu, Kata ya Mtindiro

Mgombea Ubunge Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema  watabadilisha matumizi ya soko lililojengwa katika Kijiji cha Mtindiro na kuweka kituo cha baridi (Cold Room) ili kukusanya machungwa ya wakulima kabla ya kuuzwa.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Mtindiro, MwanaFA alisema ili kuongeza thamani ya machungwa na kukabiliana na tatizo la machungwa kuoza kabla ya kuuzwa, wakulima watayahifadhi katika kituo hicho na baadae kuyauza.

Alisema kiasili kata ya Mtindiro imekuwa na wakulima wengi wa machungwa lakini tatizo kubwa ni kuharibika kabla hawajauza hivyo kuhifadhia katika kituo hicho kutawafaidisha wakulima wengi.

Alisema kituo hicho pia kitasaidia kupatikana wanunuzi na wakulima wataondokana na tatizo la kuwekeza machungwa yao kwa madalali ambao wamekuwa wakiwekeza katika vipindi vyote vya Msimu.

Aliwataka wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwenda kupiga kura kuchagua wagombea wa CCM ambao katika miaka mitano iliyokwisha wameonesha dhamira ya kusukuma maendeleo yao.

"Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ndugu zangu anastahili kuchaguliwa tena, kata yenu ameleta fedha nyingi zilizotekeleza miradi mingi ya maendeleo kuliko wakati wowote ule," alisema na kuongeza,

"Ndugu zangu Rais anayodhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo mpigieni kura, na mimi kijana wenu halkadhalika na diwani wenu Musatapha Khatibu," alisema.

Alitaja fedha zilizopelekwa katika kata hiyo kuwa ni shilingi milioni 900 ambapo katika shule ya sekondari zilipelekwa kiasi cha shilingi milioni 205 ambazo zimejenga madarasa, vyoo, ofisi za walimu na nyumba za walimu.

Elimu ya msingi walipata shilingi milioni 186.5 iliyokarabati miundombinu ya shule.

Alisema katika suala la afya zahanati ya Kijiji hicho ilipata shilingi milioni 20 na katika Umeme vitongoji vyote 13 vimepata Umeme.

Kwa upande wa barabara jumla ya shilingi milioni 200 ambazo zilifanyia matengenezo ya barabara za kata hiyo kwa kurekebisha sehemu korofi ingawa alikiri kwamba tatizo za barabara nyingi zimekuwa korofi.

Kuhusu Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) alisema awali Kijiji kimoja kilikuwa na wanufaika lakini Sasa wanufaika wapo katika vijiji vyote.

"Ndugu zangu kutokana na huruma ya Rais wetu zoezi hili litafanyika tena kwenye vijiji vyote, naomba mteteane ili wapatikane wanufaika wengi kama dhima ya serikali kusaidia kaya masikini," alisema.

Akizungumza malengo yake ya miaka mitano ijayo MwanaFA alisema:

* Miradi yote iliyoanzishwa katika kata hiyo ikiwemo changamoto zilizopo anakwenda kushughulika nazo na zitakuwa ni kipaumbele chake.

* Kuhakikisha wanapata kituo cha afya na zahanati moja

* Ujenzi wa sekondari ya kidato cha Tano na sita pamoja na ujenzi wa mabweni ya wasichana na wavulana

* Kukarabati barabara za kata hiyo na 

* Kuanzisha kituo cha kukusanyia na kuhifadhi machungwa

Post a Comment

0 Comments