MWANA FA KATA YA MAGOROTO

Na Mwandishi Wetu, kata ya Magoroto

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema jukumu kubwa walilonalo wananchi wa kata ya Magoroto ni kumchagua Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuingoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 29.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Miembeni, MwanaFA alisema Mama Samia anayodhamira ya dhati ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hapa nchini.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano aliyohudumu kama Mbunge wa Muheza, Rais Dkt Samia alileta jumla ya shilingi bilioni 1.4 ambazo zimegharamia miradi mbalimbali ya Elimu, afya na barabara katika kata hiyo, hivyo anastahili kupigiwa kura nyingi za ndiyo.

"Ndugu zangu wa Magoroto nawaomba mkampigie kura Dkt Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha miaka mitano ameleta fedha nyingi ambazo zimetekeleza miradi yenu," alisema na kuongeza,

"Hata mngekuwa na diwani anasema kama chiriku au mbunge mwenye kimbelembele kiasi gani lakini kama Rais hasikii vilio vyenu hakuna fedha itakuja,".

"Ndiyo maana sisiti kusimama mbele yenu kumwombea kura Rais Dkt Samia kwasababu mama huyu ni msikivu, shida tunazomweleza zinamgusa na anatoa fedha ili ziweze kuwarahisishia maisha yenu ndugu zangu," alisema.

Aeleza kazi alizozifanya kata ya Magoroto

Kwa upande wa elimu ya sekondari MwanaFA alisema zililetwa jumla ya shilingi milioni 205 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Mlinga.

Kwa upande wa elimu ya msingi jumla ya shilingi milioni 798.5 ambazo zilitumika katika shule za Miembeni, Gare, Misufini na Mgambo.

"Hakuna kitu kinanipa usingizi kama Ile shule ya msingi tuliyojenga pale Misufini, hata Rais alipokuja nilimwambia serikali isiingize fedha yoyote nitaimaliza mwenyewe ili siku nikiacha kazi hii nikae na wajukuu zangu niwahadithie kuhusu hili," alisema.

MwanaFA pamoja na marafiki zake wamejenga vyumba vinne vya madarasa, vyoo na ofisi ya mwalimu katika shule hiyo iliyopo Kijiji cha Misufini kwa gharama ya shilingi milioni 350 ambapo wananchi Sasa kupitia diwani wao wanataka iitwe MwanaFA Shule ya Msingi.

MwanaFA alieleza namna alivyosukumwa hadi kuijenga shule hiyo wakati anafika katika Kijiji cha Misufini mwaka 2020 kuomba kura, alisindikizwa na watoto ambao walikuwa wakimuimbia nyimbo za changamoto yao ya kusoma mbali ya Kijiji chao hivyo akaweka nadhiri kutatua changamoto hiyo.

"Roho iliniuma sana kuona nasikindikizwa na watoto wakiimba kueleza changamoto yao huku wakiwa na furaha pamoja na bashasha, niliweka nadhiri nijenge shule hii kweli Mimi na marafiki zangu tumeanza kujenga vyumba vinne," alisema na kuongeza,

"Hili la jina tuliache kwanza halafu tutajadiliana muda ukifika, tunataka kwanza watoto wasome,".

Kwa upande wa maji alitafuta wafadhili ambao walileta shilingi milioni 14 kwa ajili ya uchimbaji kisima Kijiji cha Miembeni.

Kwa upande wa barabara alisema zililetwa shilingi milioni 100 ambazo zimechonga barabara inayoelekea katika kata hiyo na kuwekwa zege katika maeneo korofi.

Hata hivyo, alisema kuwa kata hiyo ambayo Ina vivutio vya utalii atahakikisha anaendelea kutafuta fedha ili wageni wengi wa ndani na nje wanaokwenda kutalii wafike kwa wingi ili kuinufaisha kata hiyo pamoja na Muheza kwa ujumla.

Umeme alisema wakati akiingia vijiji vitano kati ya Saba na vitongoji 30 kati ya 34 havikuwa na Umeme lakini Sasa vimebaki vitongoji 10 pekee ambavyo tayari vingizwa katika mpango wa kuwekwa Umeme katika bajeti ya mwaka huu.

Kwa upande wa afya shilingi milioni 32.5 zililetwa ambazo zilikwenda kuboresha zahanati ya Miembeni  na kuanza ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Magomba.

Mfuko wa Jimbo uliweza kuhudumia mambo mbalimbali ikiwemo kupeleka shilingi milioni 2.5 shule ya sekondari Mlinga kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta na printer yake lakini pia shule ya msingi Mgambo ilipata shilingi milioni 1.4 ambayo ilinunulia bati 50.

Mambo atakayoyafanya endapo atachaguliwa tena katika kata hiyo

Kusimamia miradi yote ilianzwa na serikali katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na Umeme.

Kutobadilisha dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Magoroto, atafanya kazi kwa kiwango kikubwa hasa kwakuwa Sasa anakwenda kufanya kazi ya ubunge kutoka miaka yake mitano ya kujifunza na 

Atahakikisha uwanja wa michezo ulioanzwa katika kata hiyo unamalizika na vijana wanafurahia kwa kucheza na kuibua vipaji vyao.

"Niwaombe katekelezeni jukumu lenu la kwenda kutupigia kura mchagueni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mimi kijana wenu na Kisha mumpigie kura za ndiyo diwani wenu kwakuwa yupo mwenyewe," alisema.

Akizungumza katika mkutano huo Mgombea udiwani wa kata hiyo Yohana Mwakapokela aliwaambia wananchi wa Magoroto hana cha kuwalipa bali anakwenda kushirikiana na Rais, MwanaFA kuwaletea maendeleo na akawata watimize jukumu lao la kuwapigia kura wagombea wa CCM.

Alisema wananchi wa kata hiyo wamuamini mbunge MwanaFA kwakuwa tangu Muheza iumbwe kata hiyo haijawahi kupata  fedha zake za mfukoni mbunge hata shilingi milioni tano kuwapa kwa ajili ya maendeleo lakini MwanaFA amewapa shilingi milioni 350 akawajengea shule.

"MwanaFA fedha hizo angeweza kujenga shule pale Muheza mjini akapiga pesa lakini kwa kututhamini wananchi wa Magoroto amezileta na ametujengea shule," alisema na kuongeza, 

"Kwaheshima na taadhima na kwa ridhaa yako shule Ile uliyojenga, isajiliwe MwanaFA Shule ya Msingi Misufini, kwasababu tangu Muheza iumbwe hakuna mbunge aliyetupa hata shilingi milioni tano akasema Magoroto fedha hii ifanyeni maendeleo isipokuwa wewe,".

Mgombea huyo alisema katika kata yao jumla ya sh. 1,477,400,000 zililetwa katika kata hiyo kwa ajili ya miradi ya Maji, elimu, barabara na afya hivyo shukrani zao za pekee ni kuipa jina la MwanaFA  shule hiyo kama shukrani zao lakini pia wanaahidi watapiga kura za mafuriko ili kata hiyo iongoze kwa kura kati ya kata 37 zilizopo wilayani Muheza.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa mkoa wa Tanga, Biumrah Juma Sekiboko aliwanadi wagombea wa CCM Rais, mbunge na diwani akizungumza na ndugu zake wa Magoroto Kisambaa.

"Wanaume na wanawake na vijana wenzangu, nawaomba sana wote twendeni tukapige kura tatu tumchague Rais, MwanaFA na diwani, CCM ni chama chenye mapenzi makubwa na watu wake nawaomba kwa ridhaa yenu twendeni tukawachague, wakashirikiane kutuletea maendeleo," alisema Biumrah.

Alisema anawaombea kura kwasababu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama ambacho kimekuja na ilani ambayo ndiyo msingi na mwongozo wa wagombea hao katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments