Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Kassim Amari akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni Kata ya Makorora
*************
TANGA MJINI
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim
Amari, amewaahidi wananchi wa Tanga Mjini kuwa atahakikisha Soko la Makorora
linakamilika kwa wakati, jambo ambalo litaleta tija kwa wafanyabiashara na
wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya
Makorora, Amari alisema soko hilo litawawezesha wafanyabiashara kufanya
biashara katika mazingira salama na yenye mpangilio wa kisasa.
“Soko la Makorora ni
miongoni mwa miradi iliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2025–2030, hivyo ni lazima likamilike kwa wakati,” alisema Amari.
Aliongeza kuwa Soko la Mlango wa Chuma pia litajengwa kuwa
soko la kisasa, huku Soko la Mgandini likibadilishwa kabisa na kuwa na sura
mpya itakayovutia wananchi na wafanyabiashara.
Mgombea huyo pia alisema kuwa ili kupunguza kero
zinazotokana na bili kubwa za maji, wakazi wote watabadilishiwa mita za maji na
kufungiwa mita za luku za maji, zitakazowawezesha kulipia matumizi kulingana na
kiasi wanachotumia.
Amari alisisitiza kuwa CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia
Suluhu Hassan inajipanga kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kupitia miradi inayoleta
manufaa kwa wananchi moja kwa moja.
Aliwaomba wananchi wa Tanga Mjini kuichagua CCM kuanzia
ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais ifikapo Oktoba 29,akisisitiza kuwa ahadi
zote zilizopo katika kampeni zinaungwa mkono na ilani ya chama hicho.
0 Comments