Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeeleza kuwa linaendelea kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa nchini, huku wajasiriamali wadogo na wa kati wakihimizwa kutoiogopa TBS, kwani shirika hilo lina mpango maalumu wa kuwasaidia ili waweze kukuza biashara zao na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Hayo yameelezwa na Afisa Uthibiti Ubora Mwandamizi wa TBS,Kaiza Kilango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika mkoani Tanga.
Kaiza amesema kuwa wajasiriamali wadogo na wa kati wanatakiwa kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili kupata mafunzo kuhusu kanuni bora za uzalishaji pamoja na usafi wa mazingira katika utengenezaji wa bidhaa zao.
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao ili bidhaa wanazozalisha ziweze kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, jambo litakalowawezesha kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha taratibu za SIDO, mjasiriamali atatakiwa kujaza fomu maalumu ya kutathmini mtaji wake. Endapo mtaji wake wa uzalishaji (ambao unahusisha mashine na rasilimali watu, lakini haujumuishi jengo) utakuwa chini ya shilingi milioni 75, basi serikali itamuweka katika kundi la mjasiriamali mdogo na wa kati.
Aidha,Kaiza amewataka wajasiriamali kutumia fursa zilizopo TBS, ikiwemo huduma za usajili wa bidhaa, vipimo na ithibati, ambazo sasa zinapatikana katika mikoa yote nchini, badala ya kusafiri hadi makao makuu ya shirika hilo.
Kwa upande mwingine, amewahimiza kuzingatia kanuni za usalama wa chakula na matumizi sahihi ya vifungashio ili kulinda afya za watumiaji na kuongeza thamani ya bidhaa zao sokoni.
0 Comments