Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kujenga reli ya kisasa ya SGR katika Mkoa wa Tanga, ambayo itakuwa na urefu wa kilomita 1,108.
Reli hiyo itapita katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida na Musoma ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya usafiri nchini.
Akizungumza wakati wa kampeni za ubunge zilizofanyika katika Jiji la Tanga, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Amari, alisema mradi huo ni wa kimkakati na unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kassim alisema kuwa Serikali Kuu tayari imeweka mpango wa kuhakikisha ujenzi wa reli hiyo unatekelezwa kwa viwango vya kimataifa, ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alifafanua kuwa treni zitakazotumika kwenye reli hiyo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria na mizigo kwa wakati mmoja, jambo litakalopunguza gharama za usafiri na kuongeza tija katika sekta ya biashara.
Kwa mujibu wa Kassim, ujenzi wa reli hiyo utasaidia pia kufungua fursa za ajira kwa vijana wengi, hasa wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika kwa mradi huo.
Aliongeza kuwa maendeleo hayo yataongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa kutoka bandari ya Tanga kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na hata nchi jirani.
Katika upande wa kijamii, Kassim alisisitiza kuwa moja ya kipaumbele chake ni kuhakikisha vijana kutoka familia zenye kipato cha chini wanapata mikopo itakayowawezesha kujitegemea kiuchumi.
Alisema mikopo hiyo itawalenga zaidi vijana wanaomaliza kidato cha sita na wale waliopo mitaani wasiokuwa na ajira, ili waweze kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi.
Kassim pia aliahidi kushirikiana na viongozi wa mitaa na serikali za mitaa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo kusaidia mayatima, wajane na makundi mengine yenye uhitaji maalum.
Alibainisha kuwa viongozi wa mitaa wana nafasi kubwa katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia walengwa, hivyo atahakikisha anashirikiana nao kwa karibu.
Aidha, mgombea huyo wa ubunge alisema atahakikisha Kituo cha Afya cha Makorora kinaboreshwa kwa kuongeza vifaa tiba vya kisasa, ili wananchi wapate huduma bora za afya bila kusafiri umbali mrefu.
Mwisho wa hotuba yake, Kassim Amari aliwahimiza wananchi wa Jiji la Tanga kuhakikisha wanachagua wagombea wa CCM katika ngazi zote, akisema, “hakikisheni mnachagua mafuga matatu — diwani, mbunge na rais — msije mkaweka magunzi katikati.”
0 Comments