TBN YAPONGEZA VYAMA VYA SIASA KWA KAMPENI ZA KIUNGWANA

MTANDAO wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network – TBN) umepongeza Watanzania kwa kukamilisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani, utulivu na uzalendo, huku ukitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kesho Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Katika taarifa iliyotolewa leo Oktoba 28,2025 jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, mtandao huo umeeleza kuwa kampeni za mwaka huu zimekuwa za mfano bora wa kisiasa barani Afrika kutokana na kuendeshwa kwa heshima, hoja na kufuata sheria za uchaguzi.

“TBN inatoa pongezi za dhati kwa Watanzania wote, wagombea, vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wadau wote kwa kukamilisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mazingira ya amani na utulivu yaliyotawala kote nchini,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

TBN imesisitiza kuwa hakuna matukio makubwa yaliyoweza kuhatarisha amani ya nchi, jambo linalothibitisha ukomavu wa kisiasa wa Watanzania na heshima kwa kanuni na maadili ya uchaguzi.

“Amani yetu ni urithi na hazina kubwa. Mwenendo wa kampeni za mwaka huu umethibitisha kwamba Watanzania wanaiweka amani na maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kisiasa,” amesema Msimbe

Mtandao huo umewahimiza wananchi wote waliojiandikisha kuhakikisha wanatumia siku ya mapumziko iliyotangazwa rasmi na serikali kwa ajili ya uchaguzi kufanya maamuzi sahihi kwa kupiga kura.

“Kura yako ni sauti yako ya kuweka msingi wa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu,” imeongeza taarifa hiyo.

Aidha, TBN imetoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani na umoja wakati wa kupiga kura na kusubiri matokeo, huku ikieleza matumaini kuwa uchaguzi huu utazaa matokeo yanayojenga imani na matumaini mapya kwa taifa.

“Tanzania Bloggers Network (TBN) inawatakia Watanzania wote uchaguzi mwema na wa mafanikio, tukitarajia matokeo yatakayojenga matumaini makubwa kwa taifa hili katika safari yake ya kuelekea maendeleo endelevu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu bariki amani yetu.”

Post a Comment

0 Comments