Vyama vya kisiasa nchini Kenya viko kwenye hatari kwa wagombea wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kuondolewa katika orodha ya wagombea iwapo vyama hivyo havitatimiza mahitaji ya sheria ya usawa wa jinsia tume ya uchaguzi Kenya (IEBC) imetangaza.
Vyama hivyo vinakabiliwa na ugumu wa kutimiza mahitaji ya usawa wa jinsia katika usajili wake wa wagombea watakaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu baadae mwaka huu baada ya IEBC kukariri kuwa sheria inayohitaji jinsia moja kutokuwa na zaidi ya theluthi mbili ya viti vya bunge na nafasi nyingine za uteuzi ni sharti itimizwe baada ya vyama hivyo kufanya kura ya mchujo kuwapata wagombea.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari,tume hiyo imeeleza kuwa itatupilia mbali orodha ya wagombea kutoka chama fulani cha kisiasa iwapo idadi ya wagombea wa kiume ni wengi mno kupita kiasi kuliko idadi ya wagombea wa kike.
Katika barua hiyo IEBC inaeleza kuwa ikitokea chama cha kisiasa kitawasilisha orodha wa wagombea 290 wa nafasi ya ubunge kulingana na nafasi za kuchaguliwa,si zaidi ya wagombea 193 wanastahili kuwa wa jinsia moja.
Pia ikitokea kuwa chama cha kisiasa kitawasilisha orodha inayojumuisha wagombea 47 wa bunge la Seneti sio zaidi ya wagombea 31 wanastahili kuwa wa jinsia moja.
Vile vile ikitokea kuwa chama cha kisiasa kitawasilisha orodha inayojumuisha wagombea wasiofikia idadi ya maeneo yanayogombewa, sheria ya jinsia moja bado itatumika.
Kufikia leo Ijumaa vyama vya kisiasa nchini Kenya vinastahili kuwa vimewasilisha orodha hiyo ya wagombea lakini tume ya uchaguzi imetoa maelezo kuwa itavipa vyama hivyo saa 48 kurekebisha orodha kuafiki mahitaji ya sheria na iwapo bado vyama hivyo vitawasilisha orodha isiyofikia sheria hiyo orodha hiyo ya chama husika itaondolewa kabisa na chama hakitahusika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Maagizo ya IEBC yananuia kuwiana na maamuzi yaliotolewa na mahakama kuu kuitaka tume hiyo kufuatilia sheria ya jinsia katika uchaguzi mkuu kutii kanuni hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imeibua utata tangu kutekelezwa kwa Katiba ya 2010.
Agatha Soltei ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uteuzi katika chama cha Wiper Democratic Movement ameeleza kuna ugumu wa kuafiki sheria hiyo maana si idadi nyingi ya wagombea wa kike wamejitokeza kushiriki mchujo wa vyama au kushikilia nafasi za kisiasa.
Bunge la Kenya wakati wote limekuwa katika hatari ya kuvunjwa baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kumuandikia rais Uhuru Kenyatta kulivunja kwa kushindwa kutimiza sheria ya usawa wa jinsia, katika zaidi ya kipindi cha miaka mitano baada ya katiba kuidhinishwa mwaka 2010.
Hata hivyo,Kenyatta alighairi ushauri huo hatua iliyolifanya bunge hilo kuelekea mahakamani kutafuta ufafanuzi zaidi na kumdhibiti rais Kenyatta kulivunja.
0 Comments