Baraza la Uwezeshaji Lasifu Ushiriki wa Wananchi Katika Miradi Tanga

Watanzania wameendelea kuonesha uzalendo wao kwa kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Mkoa wa Tanga, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya miradi hiyo pamoja na ustawi wa wananchi,ushiriki huo umejikita katika kulinda,kusaidia na kushiriki moja kwa moja katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na miradi hiyo.

Katika hali hiyo,wananchi wa maeneo yanayozunguka miradi hiyo wamekuwa wanufaika wakubwa wa fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo ajira na biashara ndogo ndogo zinazochipuka kutokana na uwepo wa miradi hiyo. Hali hii imeongeza kipato cha kaya nyingi na kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limebainisha kuwa ushirikiano huo kati ya wananchi na wawekezaji ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Ushirikiano huo pia husaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga, Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa Aurelia Kamzora, alieleza kuridhishwa na namna wananchi wanavyoendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amesema kuwa miradi mikubwa kama hiyo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa, kwani huongeza mzunguko wa fedha katika jamii na kutoa fursa kwa wazawa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Profesa Kamzora alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya faida za miradi hiyo ili waweze kuilinda na kuithamini, jambo litakalosaidia kuhakikisha inatoa matokeo chanya kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo, Gwakisa Bapala, alisema kuwa mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Chongoleani na maeneo ya jirani, hasa kupitia ajira zinazotolewa wakati wa ujenzi na uendeshaji.

Alibainisha kuwa zaidi ya watu 1,800 wamepata ajira kupitia mradi huo, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi wa eneo hilo.

Aidha, alisema kuwa pamoja na ajira, mradi huo umechochea ukuaji wa biashara ndogo ndogo kama vile huduma za chakula, usafirishaji na makazi, ambazo zimekuwa zikiwasaidia wananchi kujipatia kipato cha ziada.

Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Tanga umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ushirikiano wa wananchi ukiendelea kuwa msingi muhimu wa mafanikio ya miradi hiyo.

Post a Comment

0 Comments