Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, ameitaka Serikali kuweka sheria kali zaidi za kudhibiti migogoro ya ardhi pamoja na matumizi holela ya maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma nchini.
Akizungumza bungeni, Baba Levo amesema migogoro mingi katika jamii imekuwa ikichangiwa na masuala ya ardhi, huku baadhi ya maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa huduma za jamii yakibadilishwa matumizi kinyume cha utaratibu.
Amesema ardhi ni moja ya mambo yanayosababisha migogoro mikubwa katika jamii kutokana na umuhimu wake kwa maisha na maendeleo ya wananchi.
“Ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro. Tunaona maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa matumizi ya umma yakibadilishwa matumizi kila mara. Serikali ina mpango gani wa kuweka sheria kali kudhibiti hali hii?” amehoji Baba Levo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaovamia maeneo ya wazi au kufanya ujenzi bila kufuata sheria na mipango ya matumizi ya ardhi.
Mmuya amesema Serikali haitasita kubomoa majengo yote yaliyojengwa kinyume cha sheria katika maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma bila kujali gharama zilizotumika.
Aidha, amewataka wananchi kuhakikisha wanapata vibali halali vya ujenzi na kufuata sheria za mipango miji ili kulinda maeneo ya wazi na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

0 Comments