Wananchi Tanga Kushiriki Kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mara ya Kwanza

Wakazi wa Jiji la Tanga wanatarajiwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika kuukimbiza na kuushika Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni utaratibu mpya unaolenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za mwenge.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amesema Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu ni wa kipekee kwa kuwa wananchi watapewa nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika mbio za mwenge tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyopita.

Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika shughuli hiyo ambayo inalenga kuimarisha uzalendo na kuwaleta wananchi karibu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

“Mwenge wa safari hii ni mwenge wa watu,ushiriki wa wananchi kuushika na kuukimbiza ni mkubwa zaidi,tunahitaji wananchi wajitokeze kwa wingi ili washiriki katika kuukimbiza"amesema Kolimba.

Halmashauri ya Jiji la Tanga inatarajiwa kuupokea Mwenge wa Uhuru Juni 21 kutoka Wilaya ya Pangani, ambapo utakimbizwa kwa umbali wa kilomita 58.9 kuanzia eneo la Tundaua lililopo Kata ya Kirare.

Katika ziara yake ndani ya Jiji la Tanga, Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 3.6.

Miongoni mwa miradi hiyo, miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 itawekewa mawe ya msingi, miradi mingine miwili yenye thamani ya shilingi milioni 700 itafunguliwa rasmi, huku miradi miwili yenye thamani ya shilingi milioni 300 ikikaguliwa ili kutathmini utekelezaji wake na manufaa kwa wananchi.

Kolimba amesema maandalizi yote ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yamekamilika na ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Tanga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo muhimu la kitaifa pamoja na kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika jiji hilo

Post a Comment

0 Comments