WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA AWAPA SAA 72 VIKOSI VYA TPLF KUJISALIMISHA.

                                                    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema majeshi ya nchi hiyo yamechukua udhibiti wa mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle.

Abiy ametangaza kuwa serikali ya shirikisho sasa imechukua udhibiti kamili wa mji huo ikiwemo uwanja wa ndege, taasisi za umma, ofisi za utawala wa jimbo hilo na maeneo mengine muhimu.

Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumamosi, Abiy ametangaza pia kuwa wamemaliza operesheni yao ya kijeshi katika jimbo hilo.

Abiy ameongeza pia kuwa maelfu ya wanajeshi ambao walikamatwa na wapiganaji wa chama tawala katika jimbo hilo ‘Tigray People's Liberation Front'- TPLF, yaani Chama cha Ukombozi wa Watigray pia wameachiliwa huru. Chama cha TPLF kimekuwa madarakani katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.

Jumamosi, mkuu wa majeshi wa Ethiopia Jenerali Berhanu Jula alisema baada ya vikosi vyake kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Mekelle, sasa wanawasaka wapiganaji wa TPLF wanakojificha.

Machafuko ya jimbo la Tigray yalianza mapema mwezi huu wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019, alipoviamrisha vikosi vyake kuanza operesheni kwa lengo la kuuondoa uongozi wa jimbo la Tigray.

Chama cha TPLF kimetawala siasa za Ethiopia kwa miaka mingi, lakini tangu Abiy Ahmed alipochukua madaraka mnamo mwaka 2018, amekuwa na msuguano na viongozi wa Tigray.

Pande zote mbili zimeripoti kuhusu mauaji lakini kufuatia kuzimwa kwa intaneti pamoja na huduma za mawasiliano ya simu kukatizwa, imekuwa vigumu kupata tarifa kamili ya vifo kuhusiana na machafuko hayo ya Tigray, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kadhaa ya angani na kisa kimoja cha mauaji ya halaiki ambapo mamia ya watu waliuawa.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na zaidi ya Waethiopia 40,000 wamekimbia vita na kuingia Sudan.

Post a Comment

0 Comments