Na Paskal Mbunga, Tanga.
BAADHI ya wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wanaozoa taka mitaani wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko kutokana na baadhi yao kuzoataka na kupakia kwenye gari la usafi kwa kutumia mikono wazi bila kuvaa kinga ya mipira ya mikono (Gloves)na gari la usafi libeba uchafu likiwa wazi bila kufunikwa.
Hali hiyo inawashangaza wenyeji wa Jiji hilo walioshindwa kuamini macho yao wanapowaona wazoa taka hao wakiingiza mikono yao ikiwa wazi kwenye madimbwi ya taka,nyingine zikiwa zimeoza na kutoa harufu mbaya.
Wakizungumza na waandishi habari mwanzoni mwa juma hili baadhi ya wakazi hao walisema kwamba licha ya kuzoa taka kwa mikono,lakini pia magari yao ya kuzoa taka yapo wazi,hayafunikwi.
Walisema kitendo kinachosababisha taka zilizoko garini kupeperushwa na upepo na hivyo kuzifanya zizagae ovyo mitaani na kuhatarisha afya za wakazi wa Jiji.
"Adha hii ya harufu mbaya mitaani Itaisha lini maana imekuwa ni kero kubwa sana katika maeneo yetu ? Alihoji Juma Husseini, mkazi wa Barabara ya 16.
Naye Amina Mahaboub wa kijiji cha Ndaoya kilichoko nje kidogo Jiji la Tanga kwenye barabara ya Migogoro, alisema barabara hiyo iendayo Horohoro imechafuka kwa Uchafu unao peperushwa kutoka magari ya Jiji yanayosafirisha taka kwenda dampo kuu maeneo ya Mpirani.
Ofisa Usafi na Mazingira wa Jiji la Tanga,Kizito Nkwabi alipopigiwa simu kuulizwa hali ile anaionaje kama mkuu wa idara,alijibu kwamba masuala hayo yanawahusu zaidi maofisa Afya Kata na sio yeye.
Hata hivyo baadhi ya Maofisa Kata walipoulizwa kuhusu suala hilo walishindwa kulizungumzia kwa madai ya kuwa wao sio wasemaji bali Ofisa Usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji.
0 Comments