Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limefanya Gwaride rasmi la kuwaaga Maafisa Jenerali Wastaafu sita ambao wametimiza umri wa lazima wa kustaafu, huku Maafisa hao wakitoa wito kwa wengine waliobaki kazini kuendelea kufanya kazi kwa uweledi.
Akizungumza leo Agusti 2, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaaga Maafisa Jenerali Wastaafu sita iliyofanyika katika viwanjwa vya Twalipo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda, amesema kuwa ni sehemu ya utamaduni wa kuwaaga maafisa wastaafu ngazi ya Jenerali kwa kutambua mchango wao mkubwaa, huku akieleza kuwa wataendelea kuwatumia katika kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Jenerali Wastaafu sita , Meja Jenerali Mstaafu Gabriel Sauli Mhidze, amesema kuwa leo ni siku yake ya furaha baada ya kulitumikia Jeshi miaka 41 kwa nidhamu pamoja na uweledi mkubwa.
Maafisa Jenerali Wastaafu sita walioagwa leo ni Meja Jenerali Gabriel Sauli Mhidze, Meja Jenerali Charles Mang’era Mbuge, Meja Jenerali Ally Mzee Katimbe, Meja Jenerali Chelestino Elias Msolla, Brigedia Jenerali William Stephene Likangapa pamoja na Brigedia Jenerali Andrew Elinipenda Mughamba.
0 Comments