Na Munir Shemweta, WANMM – Mtwara
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, leo tarehe 22 Desemba 2025, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Akwilapo ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara, amesema Wizara ya Ardhi inaendelea kuchukua hatua za makusudi kushughulikia changamoto za ardhi nchini, ikiwemo zilizopo mkoani humo, kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
“Wizara itaendelea kushughulikia changamoto zote za sekta ya ardhi, na hapa Mtwara tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma stahiki,” amesema Dkt. Akwilapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amempongeza Waziri Akwilapo kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa Wizara ya Ardhi ni nyeti kwani inagusa maisha ya kila mwananchi.
“Mkoa wa Mtwara uko tayari kushirikiana na Wizara ya Ardhi katika utekelezaji wa majukumu yako kwa manufaa ya wananchi,” amesema Kanali Sawala.



0 Comments