Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha malezi bora ya watoto na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi maalum, ikisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la pamoja la familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Desemba 22, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na fursa kwa makundi maalum kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu ya malezi na makuzi bora ya watoto ili kujenga kizazi chenye maadili mema na uzalendo.
Dkt.Gwajima amesema kupitia Mwongozo wa Wajibu wa Wazazi na Walezi, Serikali inaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa baba na mama katika malezi ya watoto, kwa lengo la kuhakikisha ukuaji timilifu wa mtoto kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Ameongeza kuwa Serikali inatekeleza Programu ya Malezi ya Vijana Balehe (Furaha Teen) katika mikoa ya Songwe na Mbeya, inayolenga kuwawezesha wazazi kuwaongoza vijana wao katika kipindi cha balehe na kuzuia mmomonyoko wa maadili pamoja na tabia hatarishi.
Kuhusu mapambano dhidi ya ukatili, Waziri Gwajima amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza kampeni za kijamii za kuelimisha jamii, kukemea na kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, hatua iliyoongeza uelewa na kurahisisha utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalamu wakiwemo maafisa ustawi wa jamii, walimu wa unasihi, wahudumu wa afya na polisi jamii ili kuhakikisha waathirika wa ukatili wanapata huduma za ulinzi, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kuanzia ngazi ya jamii.
Aidha, Serikali imeendelea kusajili na kufuatilia Makao ya Watoto na Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana (Day Care Centers) ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye staha, huku jamii ikihimizwa kuanzisha na kutumia vituo hivyo.
Waziri Gwajima ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto na mapambano dhidi ya ukatili, akisisitiza kuwa mtoto anayelelewa katika mazingira salama na yenye upendo ni msingi wa Taifa lenye amani na maendeleo ya kijamii.

0 Comments