Uturuki Yaongeza Ushirikiano wa Kijeshi na Nchi za Afrika

Uturuki imeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya Afrika katika mafunzo ya kijeshi na usaidizi wa kiufundi, kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na kuimarisha usalama na uthabiti wa bara hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yaşar Güler, wakati wa mkutano na wawakilishi wa mashirika ya habari uliofanyika jijini Ankara mwishoni mwa wiki, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya wizara yake.

“Kuhusu Afrika, kuimarisha ushirikiano wetu wa ulinzi na mataifa ya Afrika ambayo tuna uhusiano wa kihistoria na kitamaduni nayo, na kuchangia usalama na uthabiti wa bara hilo, bado ni miongoni mwa vipaumbele vyetu,” amesema Güler.

Ameeleza kuwa kulingana na maombi yanayopokelewa, Uturuki inaendelea kutoa mafunzo, ufadhili, vifaa na msaada wa kiufundi kwa majeshi ya nchi mbalimbali za Afrika ili kuimarisha uwezo wao wa kiusalama. Katika muktadha huo, Uturuki pia inaendesha programu za mafunzo ya lugha ya Kituruki kwa nchi 12 za Afrika ambazo ni Somalia, Libya, Senegal, Gambia, Burkina Faso, Cameroon, Mali, Djibouti, Nigeria, Niger, Gabon na Guinea, kupitia Wizara ya Ulinzi, Wakfu wa Maarif wa Uturuki na Taasisi ya Yunus Emre.

Libya yenye umoja

Akizungumzia juhudi za Uturuki nchini Libya, Waziri Güler amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili, akiielezea Libya kama jirani wa Uturuki katika eneo la Mediterania, huku akihakikishia kuendelea kwa dhamira ya Uturuki katika kulinda amani.

“Mafunzo ya kijeshi, usaidizi, ushirikiano na shughuli za ushauri za Uturuki nchini Libya zinaendelea kwa lengo la kuimarisha uhuru, umoja wa kisiasa, amani, utulivu na uthabiti wa nchi hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa masuala ya baharini kati ya nchi hizo mbili umejengwa juu ya makubaliano ya mwaka 2019 kuhusu maeneo ya bahari, ambayo sasa yamepanuliwa kujumuisha sekta nyingine zikiwemo ulinzi wa nishati na mapambano dhidi ya uhamiaji haramu.

Post a Comment

0 Comments