Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewapa siku saba Mameneja wa TANROADS na TARURA Mkoa wa Lindi kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la haraka kuhusu ujenzi wa daraja katika eneo la Congo, lililopo kwenye barabara ya Nachingwea–Masasi.
Agizo hilo limetolewa Jumapili Desemba 21,2025,wakati Waziri Mkuu akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Nachingwea mara baada ya kukagua ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
“Nawapa siku saba mje na suluhisho la daraja la dharura. Kuanzia kesho wekeni mpangokazi wa kuokoa hali hii. Mkuu wa Mkoa nipatie taarifa kwamba mmekaa, mmeamua nini na gharama ni zipi. Fanyeni kazi katika eneo la Congo na lile la Stesheni,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema barabara hiyo ilitengenezwa kwa dharura na kwa sasa inatishia usalama wa wananchi, akisisitiza kuwa ni lazima iweze kupitika wakati wakisubiri ujenzi wa kudumu.
“Kaeni na wenzenu wa TANROADS mje na suluhisho. Wananchi wanataka kupita na kupitisha mazao yao. Fanyeni haraka, msisubiri hali iwe mbaya zaidi. Barabara hii lazima ipitike, na ndiyo maana ninyi mko hapa,” aliongeza.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu maombi ya Mbunge wa Nachingwea, Bw. Fadhili Liwaka, ambaye alimuomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili eneo hilo lisilete madhara kwa wananchi hasa wakati wa mvua kubwa. Mbunge huyo pia aliomba eneo la Stesheni katika mji wa Nachingwea liwekwe makalavati ili kuzuia mafuriko.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitahidi kuhakikisha nchi ina barabara za kuunganisha mkoa na mkoa, na sasa tupo katika hatua ya kuunganisha wilaya kwa wilaya. Barabara ya Masasi–Nachingwea inatekeleza malengo yote mawili kwa kuunganisha wilaya na mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema Mbunge Liwaka.
Kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea, Mbunge huyo aliomba barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami, akieleza kuwa wako tayari kupokea ujenzi wa kilometa 20 kwa mwaka ili kupata barabara ya uhakika.
Aidha, aliomba Serikali kusaidia upatikanaji wa minara ya mawasiliano katika eneo la Kilimorondo, akieleza kuwa wakazi wake huzalisha korosho nyingi na wanahitaji huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu.
Akijibu maombi hayo, Waziri Mkuu alisema barabara hiyo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi na kuhusu minara ya mawasiliano, amesema atalichukua suala hilo na kulifanyia kazi.

0 Comments