Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imesema kuwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameongeza ufanisi na kupunguza muda wa kuhudumia meli kutoka siku saba hadi wastani wa siku tatu kwa meli moja.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwakilishi wa Meneja wa Bandari ya Tanga,Peter Milanzi, wakati wa upokeaji wa mzigo mpya wa lami kupitia Kampuni ya Wakala wa Usafirishaji ya Amura, mzigo unaosafirishwa kwenda nchini Malawi. Amesema kampuni hiyo imeamua kutumia Bandari ya Tanga kutokana na ufanisi wake mkubwa.
Milanzi alisema kuwa maboresho hayo yameifanya Bandari ya Tanga kuvutia idadi kubwa ya wateja wanaopitisha shehena mbalimbali ikiwemo magari na mizigo mingine inayokwenda katika nchi tofauti za kikanda.
“Bandari ya Tanga imeendelea kufanya vizuri kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii imewavutia wateja wengi, na leo tunapokea aina mpya ya mzigo wa lami kutoka Kampuni ya Amura. Kwa majaribio, wameleta makontena sita, kila moja likiwa na mapipa 110, yakielekea Malawi,” alisema.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo ni ishara ya kuaminika kwa bandari hiyo, na hivyo amewataka wafanyabiashara kuendelea kuitumia kutokana na huduma bora na usalama wa shughuli za upakuaji na upakiaji mizigo.
“Bandari ya Tanga ni salama na itaendelea kuwa salama. Tunatoa huduma bora na za haraka. Wale wanaokutana na changamoto katika bandari nyingine wanakaribishwa Tanga; watapata ufanisi na huduma kwa muda mfupi,” alisema Milanzi.
Ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Bandari hiyo ilipangiwa kuhudumia tani milioni 1.6. Hata hivyo, tangu mwezi Julai mwaka huu, wamekuwa wakivuka malengo kwa kuhudumia tani zaidi ya walizopangiwa—wakianza na tani 152,000, kupanda hadi 157,000, na kufikia tani 200,000 kwa mwezi kati ya Septemba na Oktoba.
Kwa upande wake, Zakaria Mohamed Nanimuka, Mwakilishi wa Kampuni ya Amura ya Dar es Salaam, alisema kuwa kutokana na ufanisi wa Bandari ya Tanga, wanatarajia kuingiza kontena nyingine 20 zitakazohudumiwa katika bandari hiyo.
“Sisi kama Kampuni ya Amura tumefurahishwa na huduma katika Bandari ya Tanga. Hakuna malalamiko wala changamoto. Tunashukuru Serikali kwa kuwekeza hapa na tutaendelea kuitumia kwa shehena mbalimbali,” alisema.
Zakaria alibainisha kuwa wamepokea shehena ya lami kutoka Iran; kontena sita zenye jumla ya tani 125 na kilo 430, kila kontena likiwa na mapipa 110. Ameishukuru bandari hiyo kwa kuwahudumia kwa wakati ikiwemo kupitisha mzigo kwenye skana bila kuchelewa.
Amesema wanatambua jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo zimeongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi katika bandari hiyo.


0 Comments