Serikali imesisitiza dhamira yake ya kulinda amani nchini, huku ikiwataka wananchi wanaotaka kufanya maandamano kufuata misingi ya sheria na taratibu zinazoongoza mikusanyiko ya umma. Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Disemba 08, 2025 na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Boniface Simbachawene, mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema maandamano yanayozungumzwa kufanyika Jumanne Disemba 09, 2025 hayajatambulishwa kisheria, hivyo ni haramu na vyombo vya ulinzi na usalama vitayadhibiti endapo yatatekelezwa bila utaratibu.
“Tunawaomba Watanzania kutoshiriki maandamano yasiyo rasmi, hasa kipindi ambacho kumekuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani na uhalifu,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene, maandamano yanayodaiwa kufanyika hayana mwombaji anayetambulika, hayana shabaha iliyoainishwa wala maelekezo ya njia za kupita, hali inayokiuka misingi ya maandamano kisheria.
Ameonya kuwa maandamano yasiyo na ukomo au yanayoelezwa kuwa makubwa kuliko yale ya tarehe 29, ambayo yaliharibu mali, kuchoma vituo vya mafuta, majengo ya serikali na kusababisha vifo, hayawezi kukubalika kwani hayana ruhusa kisheria na yana hatari ya kuvuruga amani.
“Maandamano lazima yawe na mwisho, yaombwe rasmi, yawe na taarifa ya ujumbe wake na mwelekeo ili Polisi iweze kusimamia usalama. Haya tunayoyasikia hayana vigezo hivyo,” amesisitiza.
Amehitimisha kwa kuwataka wanaotaka kutumia haki ya kuandamana kufanya hivyo kwa kufuata sheria, vinginevyo vyombo vya ulinzi na usalama vitadhibiti hali hiyo kulingana na taratibu zilizopo.

0 Comments