CCM Tanga Yatoa Maelekezo Kuboresha Usafi Soko la Mgandini


Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeliagiza Jiji la Tanga kuboresha maeneo ya kukusanyia taka katika Soko la Mgandini kwa kujaza kifusi pamoja na kurekebisha barabara za ndani, hatua inayolenga kuimarisha usafi na mazingira ya biashara.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurhaman, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi sokoni hapo, ambapo pia alisisitiza umuhimu wa kuelekeza maji ya mvua kwenye mifereji ili kuepusha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

Ziara hiyo ilikuwa ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kuboresha usafi wa soko hilo. Katika hatua hiyo, viongozi wa Jiji wameanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuondoa uchafu uliokuwepo hapo awali.

Hata hivyo, wakati wa ukaguzi huo, Mwenyekiti huyo hakuridhishwa kikamilifu na hali ya mazingira ya soko, na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha usafi unaimarika.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Rajab aliwapongeza Mstahiki Meya pamoja na viongozi wa Jiji kwa hatua walizochukua kuanza kutekeleza maagizo ya chama.

“Hatuhitaji viongozi wa kulalamika, tunahitaji viongozi wanaochukua hatua kutatua changamoto za wananchi. Mlichokifanya ni kutimiza wajibu wenu,” alisema.

Alibainisha kuwa hali ya uchafu iliyokuwepo awali haikuwafurahisha viongozi wala wafanyabiashara, na kwamba hatua zilizochukuliwa zinaonesha uwajibikaji.

Aidha, alisisitiza kuwa atarejea kufanya ukaguzi baada ya wiki mbili, huku akionya kuwa hataki kusikia visingizio badala ya utekelezaji.

“Ndani ya mwezi mmoja kuanzia Aprili 9 hadi Mei 9, tunatarajia kuona kazi imeanza. Hatutaki hadithi, tunataka vitendo,” alisisitiza.

Rajab alieleza kuwa Jiji la Tanga ni taswira ya mkoa huo, hivyo linapaswa kuwa safi na lenye mpangilio mzuri. Alikumbusha kuwa hapo awali Tanga ilikuwa miongoni mwa miji iliyosifika kwa usafi na ustaarabu, hivyo kuna umuhimu wa kurejesha hadhi hiyo.

Kuhusu huduma za vyoo sokoni hapo, Mwenyekiti huyo alieleza kutoridhishwa na hali iliyopo, akisema choo kilichopo hakikidhi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya watumiaji.

Aliongeza kuwa hali hiyo inasababisha baadhi ya watu kutumia maeneo yasiyofaa kujisaidia, jambo linalohatarisha afya za wananchi na wafanyabiashara.

Alisisitiza umuhimu wa Jiji kubuni suluhisho la kudumu, ikiwemo kuboresha mfumo wa maji taka ili kuendana na ongezeko la watumiaji.

Hata hivyo, aliwapongeza viongozi kwa kuanza mpango wa kujenga choo kipya chenye matundu 12, kitakachosaidia kupunguza changamoto hiyo, hasa katika kipindi hiki ambacho soko linatarajiwa kujengwa upya.

Kwa upande wa usafirishaji wa bidhaa, Rajab alizungumzia changamoto ya msongamano wa magari, akielekeza kuwepo kwa utaratibu maalum wa magari kuingia na kushusha mizigo kwa mpangilio.

Alipendekeza magari yapaki katika maeneo maalum nje ya soko, kisha yaingie kwa zamu ili kupunguza msongamano na kuboresha usafi.

Vilevile, alisisitiza ujenzi wa mifereji ya maji ili kuzuia maji ya mvua kutuama au kuingia sokoni, hali inayochangia uchafu na uharibifu wa mazingira.

Aliwataka viongozi wa Jiji kuwa karibu na wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa vitendo, akibainisha kuwa wananchi hao ndio chanzo kikuu cha mapato ya Jiji kupitia kodi.

Post a Comment

0 Comments