Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema yuko tayari kufanyiwa uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi ndani ya shirikisho hilo, akisisitiza kuwa hakuna cha kuficha.
Motsepe ametoa kauli hiyo Jumatano mjini Dakar, Senegal, baada ya kukutana na maafisa wa Shirikisho la Soka la Senegal pamoja na Rais wa nchi hiyo, Bassirou Diomaye Faye.
Kauli hiyo inakuja kufuatia wito uliotolewa mwezi uliopita na Serikali ya Senegal, iliyotaka kufanyika uchunguzi wa madai ya ufisadi baada ya nchi hiyo kupokonywa ubingwa wa AFCON 2025 na Bodi ya Rufaa ya CAF na kombe hilo kupewa Morocco.
Sakata hilo linahusishwa pia na matukio ya vurugu yaliyotokea Januari 18 mjini Rabat, ambapo Senegal ilishinda kwa mabao 1-0, lakini wachezaji wake walitoka uwanjani kwa muda kupinga maamuzi ya mwamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Motsepe alisema CAF iko tayari kushirikiana na uchunguzi wowote utakaoanzishwa.
“Niko tayari kwa uchunguzi kuhusu ufisadi ndani ya CAF, uwe unafanywa na serikali au taasisi yoyote. Ningependekeza hilo lifanyike, na tutatoa ushirikiano wa hali ya juu,” alisema Motsepe.
Aliongeza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni muhimu si tu katika soka, bali pia katika sekta nyingine kama biashara na siasa.
“Hatuwezi kuwaonyesha watoto wetu kuwa njia ya mafanikio ni ufisadi. Lazima tukabiliane nao kikamilifu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Motsepe alikataa kuzungumzia kwa kina mgogoro kati ya Senegal na Morocco, akieleza kuwa suala hilo kwa sasa liko katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
“Ni wajibu wangu kuheshimu mchakato wa kisheria. Suala hili liko mbele ya mahakama ya juu ya michezo duniani, hivyo siwezi kulizungumzia zaidi,” alisema.
Aidha, alipinga madai ya kuwepo kwa upendeleo kwa upande wa Morocco katika mchakato wa rufaa, akisisitiza kuwa CAF inazingatia haki na uwazi katika maamuzi yake.
Motsepe anatarajiwa kuendelea na ziara yake nchini Morocco siku ya Alhamisi kwa mikutano mingine inayolenga kuimarisha umoja na maendeleo ya soka barani Afrika.

0 Comments