Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limekabidhi eneo la ujenzi wa Kituo cha Michezo cha Kitaifa kilichopo Makatanini, katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, kwa kampuni ya ubia ya CRBC and Zhonglu Sports JV kutoka nchini China.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 29 unalenga kujenga kituo kikubwa cha michezo kitakachokuwa na miundombinu mbalimbali ya michezo pamoja na hosteli kwa ajili ya wanamichezo.
Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msita amesema mradi huo umekuwa ukipangwa kwa muda mrefu na sasa umeingia katika hatua ya utekelezaji.
Msita amesema kituo hicho kitakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania, hususan wanamichezo, kwa kuwa kitatoa mazingira bora ya mafunzo pamoja na miundombinu ya michezo ya aina mbalimbali na hosteli.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Tobias Abwao, amesema mradi huo ni fursa kubwa kwa Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla, huku akitoa shukrani kwa BMT pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuhakikisha kituo hicho kinajengwa Babati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mshauri Elekezi wa mradi huo, Beno Batinamani, ujenzi wa kituo hicho utafanyika kwa awamu tatu ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika Agosti 14, 2029 huku kukamilika kwake kukitarajiwa kuongeza fursa za mafunzo, kukuza vipaji na kuimarisha maendeleo ya michezo nchini, pamoja na kuupa Mji wa Babati nafasi muhimu zaidi katika sekta ya michezo Tanzania.

0 Comments