Mkuu wa shirika la ujasusi la Ecuador, Michele Sensi-Contugi, na mke wake, Stephany Hollihan Vasconez, ni miongoni mwa watu saba waliofariki katika ajali ya helikopta nchini Kenya siku ya Jumatano.
Serikali ya Ecuador imethibitisha vifo hivyo, huku Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo, Roberto Luque, akisema Michele na Stephany wameacha watoto na wazazi wanaopaswa kupewa pole katika kipindi hiki cha msiba.
Ajali hiyo ilitokea katika Mlima Ololokwe, Kaunti ya Samburu, takribani kilomita 270 kaskazini mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Italia, raia mwingine wa Italia na raia wa Ecuador pia walikuwa miongoni mwa watu waliofariki katika ajali hiyo.
Michele Sensi-Contugi na mke wake walikuwa nchini Kenya kwa ajili ya utalii wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipoanguka. Chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika.
Sensi-Contugi, mwenye umri wa miaka 44, alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini Ecuador kabla ya kushika nafasi ya juu serikalini. Alikuwa akimiliki na kuendesha biashara mbalimbali, zikiwemo shughuli za ndege za kitalii na uzalishaji wa bidhaa za plastiki.
Alizaliwa Desio, katika mkoa wa Monza-Brianza nchini Italia, Agosti 12, 1982. Baba yake alikuwa raia wa Italia huku mama yake akiwa raia wa Ecuador.
Baada ya kujijenga katika sekta ya viwanda, Sensi-Contugi alianza kushika nafasi mbalimbali serikalini. Umaarufu wake kisiasa uliongezeka mwaka 2024 wakati wa utawala wa Rais Daniel Noboa.
Kuanzia Aprili hadi Agosti 2024, aliwahi kuwa kaimu waziri kabla ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la ujasusi la Ecuador.
Kwa upande wake, Stephany Hollihan Vasconez alikuwa mwanamitindo maarufu nchini Ecuador na alifahamika katika sekta ya mitindo nchini humo.
Sensi-Contugi alikuwa mkuu wa shirika la ujasusi wakati ambapo serikali ya Rais Noboa ilikuwa ikiweka mkazo mkubwa katika masuala ya usalama na ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya uhalifu na usalama nchini Ecuador.

0 Comments