Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa wananchi, hususan vijana na wanafunzi, kupata maarifa na taarifa kuhusu elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema kupitia maonesho hayo, wananchi wanaweza kujifunza namna elimu na ujuzi vinavyoweza kutumika katika kukuza ubunifu, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
“Ninawakaribisha sana wananchi wa Tanga kutoka wilaya zetu zote. Hii ni nafasi ya pekee ya kuja katika maonesho haya na kujifunza mambo mbalimbali ambayo yanaweza kusaidia katika maeneo yetu,” amesema.
Maonesho hayo yamewashirikisha zaidi ya washiriki 300 kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya elimu na ufundi, shule, taasisi binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa sayansi, teknolojia na ubunifu.
Kwa mujibu wa Balozi Dkt. Burian, maadhimisho hayo pia yanatoa fursa kwa vijana na wanafunzi kufahamu vyuo mbalimbali vilivyopo nchini, kozi zinazotolewa pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya elimu na ujuzi.
Ameeleza kuwa wabunifu nao wamepata nafasi ya kuonesha kazi zao, kubadilishana uzoefu na kushindanishwa katika ubunifu, hatua inayolenga kuibua na kuendeleza vipaji vya ubunifu nchini.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ushiriki wa taasisi mbalimbali za elimu na utafiti kutoka sehemu tofauti za Tanzania unawapa wananchi fursa ya kupata taarifa mbalimbali kwa wakati mmoja na kufanya maamuzi sahihi kuhusu elimu, ujuzi na fursa za maendeleo.



0 Comments