Mamlaka nchini Morocco imewakamata wahamiaji 148 siku ya Jumamosi katika maeneo ya ndani na jirani na mji wa Fnideq, kaskazini mwa nchi hiyo, baada ya kujaribu kuvuka kwa wingi kuelekea eneo la Ceuta linalosimamiwa na Hispania, kwa mujibu wa maafisa.
Afisa wa Mkoa wa Fnideq amesema katika taarifa kwamba kati ya waliokamatwa, watu 128 walikuwa raia wa nchi mbalimbali za Afrika, huku 20 wakiwa raia wa Morocco.
Amesema uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama umewekwa katika maeneo ya karibu na Ceuta na Melilla, hali iliyosaidia kuzuia jaribio hilo la kuvuka kwa wingi. Kwa mujibu wa afisa huyo, hali ya usalama katika maeneo hayo inaendelea kuwa ya kawaida na iko chini ya udhibiti.
Mamlaka za Morocco zimesema zitaendelea kufuatilia shughuli zinazofanyika mitandaoni kwa lengo la kuwabaini watu wanaohusika katika kuhamasisha majaribio ya uhamiaji wa watu kwa wingi. Wakati huo huo, operesheni za kiusalama zinaendelea katika maeneo husika kwa ajili ya kuzuia wahamiaji kuvuka na kuwakamata watu wanaowasaidia au kuwaandaa kwa safari hizo.
Afisa huyo amesema mamlaka zimeongeza idadi ya askari pamoja na rasilimali za vifaa katika eneo hilo, ikiwemo ndege zisizo na rubani kwa ajili ya ufuatiliaji, magari ya operesheni na malori ya kubeba maji.
Jaribio hilo la kuvuka mpaka lilifanyika siku ambayo mamlaka za Morocco zilikuwa tayari zimetambua wito uliokuwa ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii wa kuwahamasisha watu kufanya vivuko vya wingi kuelekea Ceuta na Melilla.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco, Rachid El Khalfi, amesema mamlaka ziligundua hivi karibuni machapisho na jumbe zisizojulikana kwenye mitandao ya kijamii zilizokuwa zikihamasisha watu kufanya vivuko haramu vya wingi katika miji hiyo miwili mnamo Agosti 15.

0 Comments