Watafiti wa MNUAT wang’ara katika tuzo za MoEST

 

Watumishi sita wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MNUAT) wametunukiwa tuzo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) kwa kufanya tafiti zilizochapishwa katika majarida ya kitaaluma yenye hadhi ya juu kimataifa.

Tuzo hizo zimetolewa Agosti 18, 2026, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.

Watafiti waliotunukiwa tuzo hizo ni Dkt. Jofrey J. Masana, Dkt. Yusuph A. Kafula, Dkt. Abubakar S. Mgelwa, Dkt. Wambura M. Mtemi, Dkt. Mang’era S. Mnyoro na Dkt. Sekione R. Jeremiah.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Dkt. Jofrey J. Masana, ambaye ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti na Ushauri, amesema Menejimenti ya MNUAT imefurahishwa na kutambuliwa kwa watafiti hao, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya mchango wa chuo katika kukuza tafiti na ubunifu.

Amesema tuzo hizo pia zinatarajiwa kuwa chachu kwa watafiti wengine ndani ya chuo kuongeza juhudi katika kufanya tafiti zenye ubora na kuzichapisha katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa.

“Kwa upande wetu, Menejimenti ya Chuo tunawapongeza kwa tuzo hizi walizopata na tunatumai kwamba zitakuwa chachu kwa watafiti wengine wa Chuo chetu,” amesema Dkt. Masana.

Mafanikio hayo yanaendeleza rekodi ya MNUAT katika eneo la tafiti, ambapo mwaka 2024, Dkt. Jofrey J. Masana pia alitunukiwa tuzo kwa utafiti wake uliochapishwa katika jarida la kitaaluma lenye hadhi ya juu kimataifa.

MNUAT imeendelea kuweka msisitizo katika tafiti, utoaji wa elimu bora na ushauri wa kitaalamu kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuchangia maendeleo ya Taifa na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.

Chuo hicho ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga, hadi Agosti 24, 2026.

Post a Comment

0 Comments