Na Oscar Assenga, TANGA
STENDI Kuu ya Mabasi Kange, iliyopo Jiji la Tanga, inatarajiwa kuanza kutumika kwa saa 24 ndani ya wiki moja, baada ya uamuzi huo kufikiwa na uongozi wa Mkoa, Jiji na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jiji pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji kuhusu matumizi ya stendi hiyo.
Dk. Burian alisema utekelezaji wa mpango huo utaanza ndani ya wiki moja na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 8, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali katika eneo hilo ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kufanyika kwa ufanisi.
Alisema mabasi yatakuwa yakifika na kuondoka Kange, huku usafiri wa mabasi madogo, daladala na bajaji ukitumika kuwaunganisha abiria na maeneo mbalimbali ya Jiji.
“Wenye mabasi wapo tayari na wameonyesha nia ya kuanza kutumia stendi hii. Pia kutakuwa na mabasi madogo kwa ajili ya kupeleka abiria kutoka mjini kwenda Kange na kinyume chake,” alisema.

Alisema Jiji limetenga eneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari madogo ya abiria na magari binafsi, hatua ambayo itasaidia kurahisisha huduma za usafiri katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, mpango huo pia unalenga kuifanya Kange kuwa eneo muhimu la shughuli za kiuchumi, badala ya kuwa kituo cha mabasi pekee.
Alisema abiria watakaoshushwa upande mmoja wa eneo hilo watapita katikati ya kitega uchumi kilichopo Kange na hivyo kupata fursa ya kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara na wawekezaji.
“Hatuitazami Kange kama eneo la abiria pekee. Tunataka eneo hili liwe kitega uchumi na tutaendelea kuwavutia wawekezaji ili shughuli mbalimbali za kiuchumi zifanyike hapa,” alisema.
Alisema eneo hilo tayari lina taasisi na huduma mbalimbali, ikiwamo chuo cha utalii, ofisi za Serikali na baadhi ya wafanyabiashara wenye migahawa, huku jitihada zikiendelea kuwavutia wawekezaji zaidi.
Dk. Burian alisema Tanga ni lango muhimu la kiuchumi kwa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo uwekezaji katika maeneo kama Kange ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Jiji.
Alisema eneo hilo pia lina nafasi ya kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwamo harusi, mikutano na shughuli nyingine, huku Jiji na taasisi za Serikali zikitakiwa kutumia jengo hilo kwa shughuli zao na kulipia huduma hizo.
MABORESHO
Dk. Burian alisema kabla ya kuanza matumizi kamili ya stendi hiyo, maboresho kadhaa yatafanyika, ikiwamo kufanya leveling ya eneo la maegesho, kupaka rangi, kutenga eneo la ibada na kukamilisha uwekaji wa viti katika eneo la abiria.
Aidha, alisema eneo limetengwa kwa ajili ya Jeshi la Polisi kuweka vifaa na huduma zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha usalama.
Alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nalo litakuwa na gari katika eneo hilo ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama, akiwashukuru wananchi kwa juhudi za kuhakikisha mazingira ya stendi yanakuwa salama.
LATRA YAWEKA MSIMAMO
Awali, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Tanga, alisema mabasi yanayofanya safari za kimataifa yanapaswa kuzingatia utaratibu wa kutumia vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria.
Alitoa mfano wa basi linalotoka Mombasa nchini Kenya kwenda Dar es Salaam, akisema Tanga ndiyo kituo cha kwanza linapoingia nchini Tanzania.
Alisema kwa utaratibu huo, basi hilo linapaswa kuingia katika stendi ya Tanga kwa ajili ya kuhudumia abiria, huku vituo vingine vikifuata kulingana na mahitaji ya wasafiri.
Alisema uwezo wa stendi ya mkoa unapaswa kutumika ipasavyo, ikiwamo kuwezesha magari yanayofanya safari za ndani na nje ya nchi kufika kwa ajili ya ukaguzi na huduma nyingine zinazohitajika.
Alisema magari yanayofanya safari za Tanzania na nje ya nchi yataendelea kusimamiwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa na mamlaka husika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoani Tanga (TABOA) Abdi Awadhi amepongeza kutekelezwa kwa baadhi ya mapendekezo ambayo waliyatoa hapo awali huku wakiomba Serikali mabasi yote kuendelea kushusha na kupakia abiria nyakati za usiku katika stendi zao za siku zote wakati wakiendelea kuboresha miundombinu katika kituo cha Kange.
Alisema kwamba magari ya abiria yanaweza kuendelea kuanzia mjini katika kipindi cha kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi kutokana na uwezekano wa baadhi ya abiria kukosa usafiri wa daladala kuelekea Kange nyakati za usiku

0 Comments