Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Dar es Salaam ampongeza Rais Samia kwa msisitizo wa usafi.

DAR ES SALAAM – Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Razalosi Mwakiposa, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hotuba yake na msisitizo alioutoa kuhusu hali ya usafi na changamoto ya uchafu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwakiposa amesema kauli ya Rais inaonesha kuwa Serikali inatambua changamoto kubwa zinazowakabili viongozi wa Serikali za Mitaa katika kuhakikisha mazingira ya mitaa yao yanakuwa safi na salama kwa wananchi.

Amesema suala la usafi haliwezi kubebwa na viongozi wa Serikali za Mitaa pekee, bali linahitaji nguvu na ushirikiano wa pamoja kutoka Serikali, wananchi, viongozi wa mitaa, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa mazingira.

“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulizungumza kwa uzito suala la uchafu katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kauli yake inaonesha wazi kuwa anazifahamu changamoto zinazotukabili sisi viongozi wa Serikali za Mitaa,” amesema Mwakiposa.

Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa Serikali na wananchi kuunganisha nguvu katika kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa taka, utoaji wa elimu ya mazingira na kuhakikisha kila mwananchi anawajibika katika usafi wa eneo analoishi au kufanya biashara.

Mwakiposa amesema viongozi wa Serikali za Mitaa wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa kampeni mbalimbali za usafi na utunzaji wa mazingira, ili kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa mji safi, salama na wenye mazingira bora.

Amesisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na kwamba ushirikiano wa pamoja ndio utakaosaidia kupunguza uchafu katika mitaa na kuboresha afya za wananchi.

“Tukiunganisha nguvu zetu, Dar es Salaam safi inawezekana,” amesisitiza Mwakiposa.

Post a Comment

0 Comments