
Arusha, 29 Septemba 2026 — Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026), kinachofanyika jijini Arusha, kwa lengo la kupata mwelekeo na maelekezo ya kimkakati kuhusu namna taasisi za umma zinavyoweza kuongeza ufanisi, tija na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kikao hicho cha siku tatu, kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), kimewakutanisha Wenyeviti wa Bodi, viongozi wa Taasisi za Umma, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wadau wa maendeleo. Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kutoa mwelekeo wa kimkakati kuhusu mustakabali wa Taasisi na Mashirika ya Umma na kujadili hatua za kuongeza mchango wao katika uchumi na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya UNESCO, ushiriki katika kikao hicho ni sehemu ya kuendelea kushiriki katika majukwaa ya kitaifa yanayowakutanisha viongozi wa taasisi za umma kwa ajili ya kupata maelekezo ya Serikali, kubadilishana uzoefu na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ubunifu na uwajibikaji, akisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwa sehemu ya injini ya mageuzi ya kiuchumi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhe. Ndejembi pia ametoa maelekezo kuhusu uwekezaji katika vijana na ujenzi wa nguvu kazi yenye ujuzi, ambapo ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Fedha na Kilimo kuandaa mpango wa mafunzo kwa vitendo utakaowezesha angalau vijana 10,000 kupata uzoefu katika Taasisi na Mashirika ya Umma, huku vijana wengine wasiopungua 20,000 wakilengwa katika sekta binafsi.
Amesema mpango huo unalenga kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa kazi utakaowaandaa kwa fursa za ajira na kujiajiri, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa nguzo ya pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohusu rasilimali watu.
Makamu wa Rais amesisitiza pia kuwa viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma wana wajibu wa kuhakikisha kila rasilimali ya umma inatumika kwa tija, huku taasisi hizo zikibuni vyanzo endelevu vya mapato, kupunguza matumizi yasiyo na tija na kuongeza thamani kwa wananchi.
Aidha, ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha mfumo wa tathmini ya utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma, ikiwa ni pamoja na kuzingatia utekelezaji wa mpango wa kuwapatia vijana mafunzo katika tathmini za utendaji na tuzo za mwaka ujao.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, kwa kulinda miundombinu, uwekezaji wa umma na kuhakikisha huduma muhimu kwa wananchi zinaendelea kutolewa bila kuathirika.
C-CEOs Forum 2026 ni jukwaa la nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na mwaka huu limewakutanisha viongozi kutoka zaidi ya Taasisi na Mashirika 300 ya Umma pamoja na washiriki wengine zaidi ya 700. Forum hiyo inalenga kuimarisha utendaji, tija na mchango wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa kushiriki katika kikao hicho, Tume ya Taifa ya UNESCO inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuendeleza ajenda zinazohusiana na elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na taarifa, pamoja na kukuza maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo endelevu.
Ushiriki huo pia unaendana na umuhimu wa kuimarisha rasilimali watu, maarifa na ubunifu katika kufikia malengo ya Taifa, hususan katika kipindi ambacho Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
0 Comments