Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, amezindua zoezi maalumu la Msaragambo wa Mazingira litakalofanyika kila mwezi katika Mkoa huo, maarufu kama Balozi Dk. Batilda Mazingira Day, likiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki katika usafi na utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi ya mitaa na vijiji.
Akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi la usafi, Dk. Batilda alisema Mkoa umeunda kikosi kazi maalumu cha vijana 50 kitakachohusika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira, kubaini maeneo yenye changamoto ya uchafu na kuchukua hatua kwa watakaobainika kutupa taka ovyo.
Alisema kikosi hicho kitatekeleza sheria ndogo za mazingira zilizopo chini ya Halmashauri, ambapo watakaokiuka sheria hizo watakabiliwa na faini ya kuanzia Shilingi 50,000.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kikosi hicho pia kitakuwa na jukumu la kukusanya taarifa kuhusu maeneo yanayohitaji usafi na kuziwasilisha kwenye Halmashauri husika ili hatua zichukuliwe, ikiwamo kupeleka magari ya kuzolea taka.
Dk. Batilda alisema kutakuwa na kamati ya ukaguzi itakayofuatilia changamoto za mazingira, kutoa elimu na maelekezo, huku hatua za kisheria zikichukuliwa kwa watakaokaidi maelekezo na kuendelea kukiuka sheria.
Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutunza mazingira kwa hiari na kuzingatia sheria ndogo za Halmashauri, akieleza kuwa faini ya chini kwa baadhi ya makosa ya mazingira ni Shilingi 50,000.
Alisema kikosi hicho kimekaguliwa na kutambuliwa rasmi na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambalo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga litatoa ithibati na ruhusa kwa kikosi hicho kushughulikia ukiukwaji wa sheria za mazingira.
Dk. Batilda alisema faini zitakazokusanywa zitaingizwa katika mfumo rasmi wa ukusanyaji wa mapato, huku akisisitiza kuwa kikosi hicho hakitaruhusiwa kutumia nguvu wala kupokea rushwa wakati wa kutekeleza majukumu yake.
Aliwataka wananchi kushiriki kwa hiari katika zoezi hilo na kuzitaka Halmashauri zote 11 zilizopo mkoani Tanga, chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha zinatekeleza Msaragambo huo ambao umepewa jina la Balozi Dk. Batilda Mazingira Day.
Aidha, Dk. Batilda alisema Mkoa wa Tanga unachangia Shilingi bilioni sita kwa mwezi katika pato la Taifa na kushika nafasi ya sita kitaifa, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kuanzia ngazi ya kaya.
Kwa upande wake, akimwakilisha Mkurugenzi wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Meneja wa NEMC Kanda ya Bagamoyo, Ndimbumi Mboneke, alisema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama wakati wote.
Alisema wananchi pia wana wajibu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapoona uharibifu wa mazingira.
Mboneke alisema sheria ya mazingira imetoa haki kwa kila Mtanzania kuishi katika mazingira safi na salama, lakini pia imempa wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kutoa taarifa pale anapoona uharibifu.
Katika tukio hilo, NEMC ilimkabidhi cheti maalumu cha shukrani mwananchi wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Hilal, kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mustafa Seleboss, alisema Halmashauri hiyo iko tayari kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, ikiwamo kuondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga waliopanga biashara zao katikati ya stendi ya daladala.

0 Comments