DC Dadi Kolimba:Kila Mmoja Ana Wajibu wa Kuhakikisha Usalama Katika Eneo Lake

MKUU wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amewataka viongozi wa kata na mitaa kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa kutosha katika maeneo yao.

Akizungumza katika kikao cha ulinzi na usalama, Mhe. Kolimba amesema kuwa kuanzia sasa matukio yote yatakayojitokeza katika maeneo mbalimbali yatafuatiliwa kwa umakini mkubwa ili kubaini chanzo chake na hatua zilizochukuliwa na viongozi wa maeneo husika.

“Kila mmoja awajibike. Endapo tukio litatokea katika eneo fulani, tutafuatilia kwa kina tukio hilo limetokeaje, viongozi wa eneo hilo walikuwa wanalifahamu au la, na kama walilifahamu, walichukua hatua gani. Ndiyo maana tupo hapa viongozi wa Serikali na Chama, hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake,” amesema Mhe. Kolimba.

Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Watendaji wa Kata na Mitaa, Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Waheshimiwa Madiwani kutoka kata za Duga, Majengo, Chumbageni, Magaoni, Mnyanjani na Mabawa.

Post a Comment

0 Comments